Na MASHAKA MHANDO, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amefanya tukio lenye ujumbe mzito wa kiuchumi na kitamaduni baada ya kumkabidhi zawadi maalumu ya saa ya ukutani Waziri wa Vijana kutoka Zanzibar, Mhe. Suleiman Ameir, katika ufunguzi wa mkutano mkubwa wa kimataifa wa vijana unaoendelea jijini Tanga.
Mkutano huo wa kimataifa unajikita katika kujadili na kufungua fursa za vijana kupitia mpango maalumu wa kimataifa wa Global Opportunity Youth Network (GOYN), ukiwa unawakutanisha wadau mbalimbali ili kusaka mikakati ya kuwakwamua kiuchumi vijana.
Zawadi hiyo iliyomkabidhi Waziri Ameir haikuwa ya kawaida; ni saa ya kipekee iliyotengenezwa kwa ustadi mkubwa wa mikono (handicraft) ikitumia malighafi ya mkonge, zao ambalo limekuwa uti wa mgongo wa Mkoa wa Tanga.
Saa hiyo imetengenezwa na vijana wazawa kupitia kituo cha Tanga Sisal Incubation Centre, kituo kinachosimamiwa kwa karibu na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).
Akieleza sifa na maana ya zawadi hiyo, Balozi Dkt. Batilda amebainisha kuwa muunganiko wa mkonge, vifuu vya nazi, na kauri za baharini zilizotumika kupendezesha saa hiyo unaashiria utajiri mkubwa wa rasilimali asilia zinazopatikana ndani ya Jiji la Tanga.
Alisema utoaji zawadi hiyo ni mkakati wa makusudi wa kuendelea kuongezea thamani zao hilo la kihistoria la mkonge katika nyanja za sanaa na ujasiriamali.
Mwisho

Comments
Post a Comment