Meli hiyo imepinduka na kuzama disemba 26 majira ya saa Saba za usiku.
Tukio hilo limetokea meli hiyo ikiwa imefungwa katika gati la bandari ya mwanza kusini.
Kampuni ya meli Tanzania(Tashico) imethibitisha meli ya Mv. Serengeti kupinduka na kuzama upande mmoja wa nyuma.
Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma cha Kampuni hiyo inaeleza kuwa Tashico imeshirikiana na Timu mbalimbali za Wataalam kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa bandari (TPA) na wadau wengine katika Juhudi za Uokoaji.
Kwa Mujibu wa Taarifa hiyo,Taarifa rasmi ya chanzo cha Tatizo itatolewa Meli hiyo itakapokuwa imeinuliwa na Uchunguzi wa kubaini Tatizo utakapokuwa umefanyika.
Meli ya Mv.Serengeti inadaiwa kusitisha safari zake kwenye ziwa Victoria mwaka 2016
Meli ya Mv.Serengeti imepinduka na kuzama katika bandari ya mwanza kusini ikiwa ni miezi michache tangu meli nyingine ya Mv.Clarius kupinduka na kuzama katika bandari ya Mwanza Kaskazini
Meli ya Mv.Clarius ilipinduka na kuzama Usiku kuamkia mei 19 Mwaka huu ikiwa kwenye maegesho ya bandari ya mwanza Kaskazini.
Zaidi ya miezi Saba tangu kutokea kwa Tukio hilo,hakuna Taarifa zozote za uchunguzi zilizotolewa kwa umma licha ya Mamlaka inayosimamia usafiri wa majini Nchini(TASAC) kuahidi kufanya hivyo.
Baadhi ya wadau wa usafiri wa Majini kwenye ziwa Victoria wameelezea kushangazwa na hatua ya Meli ya Mv.Serengeti Kupinduka na kuzama.
Wadau hao wamehoji sababu za Meli hiyo pamoja na ile ya Mv.Clarius kupinduka na kuzama zikiwa kwenye eneo la Maegesho.
"Kinachoshangaza zaidi ni Meli zote tunaelezwa kupinduka na kuzama nyakati za Usiku tena muda unaofanana wa Majira ya Saba" alihoji Mmoja wa wadau
Aidha Wadau hao wameomba kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini na kuchukuliwa Kwa hatua stahiki kwa watakaobainika kuhusika na hatimaye kukomesha matukio hayo ambayo yameanza kuwatia hofu watumiaji wa baadhi ya vyombo vinavyotoa huduma ya Uchukuzi wa Majini katika Ziwa Victoria.