VIONGOZI WA CHADEMA- HECHE ,MZEE,MNYIKA ZINGATIENI DIPLOMASIA YA KISIASA (MAZUNGUMZO) KUMALIZA SUALA LA LISSU
Suala la Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, linahitaji busara, utulivu na diplomasia ya kisiasa (Mazungumzo ) katika kutafuta suluhu. Tunatoa wito kwa viongozi wa CHADEMA kutambua nafasi ya mazungumzo kama nyenzo muhimu ya kushughulikia changamoto za kisiasa na kujenga mazingira ya haki na maridhiano nchini.
Katika siasa, mazungumzo si ishara ya udhaifu wala kusalimu amri. Ni njia ya kidiplomasia inayowezesha pande zenye mitazamo tofauti kukutana, kusikilizana na kutafuta maeneo ya pamoja kwa maslahi ya taifa.
Tunashauri viongozi wa CHADEMA kuzingatia uwezekano wa kutumia njia za mazungumzo na ushirikishwaji, kwa kushirikiana na wadau husika, wakiwemo Serikali, katika kutafuta suluhu ya suala la Lissu kwa kuzingatia misingi ya Katiba, utawala wa sheria, haki za binadamu na haki za wahusika wote.
Ni muhimu kuelewa kuwa changamoto za kisiasa haziwezi kutatuliwa kwa kauli kali na misimamo inayofunga milango ya mawasiliano. Mazungumzo yanaweza kujenga uaminifu, kupunguza mvutano na kufungua njia ya kushughulikia tofauti zilizopo.
KKMK inaamini kuwa mustakabali wa Taifa haupaswi kujengwa juu ya uhasama wa kisiasa, bali juu ya haki, uvumilivu, uwajibikaji na kuheshimiana.
Wito wetu ni mmoja: Tufungue milango ya mazungumzo, tutangulize maslahi ya Taifa na tutumie diplomasia ya kisiasa kutafuta suluhu ya suala la Lissu na changamoto pana za kisiasa nchini.
Heche,Mzee,Mnyika ninyi ni viongozi na mnajua namna bora viongozi wanavyowasiliana,kutaneni na Rais Samia ,tambueni kwamba hoja mezani huzaa mafanikio zaidi kuliko kurushiana maneno kwenye mitandao na vyombo vya habari.
Odero Charles Odero


Comments
Post a Comment