Vijana na wanawake 289 kutoka Kata 21 za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wanatarajia kunufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa na biashara kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo.
Programu hiyo imezinduliwa rasmi katika Kata ya Bugwema, ambapo jumla ya ekari 500 zimeandaliwa kwa ajili ya kuwapatia vijana na wanawake hao fursa ya kujifunza na kujihusisha na kilimo cha kisasa chenye tija.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Musoma, Ruge Makenge, amesema ujio wa BBT ni fursa muhimu kwa vijana wa halmashauri hiyo, kwani utawawezesha kupata mashamba pamoja na mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kufanya kilimo biashara.
Amesema eneo la shamba la Bugwema lenye ukubwa wa ekari 500 limesafishwa na kugawanywa katika mashamba ya ukubwa wa ekari mbili kila moja kwa ajili ya wanufaika hao 289.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo katika Wizara ya Kilimo, Samson William Mponeja, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira ya kubadili mfumo wa kilimo nchini kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kisasa, biashara na chenye tija.
Mponeja amewataka vijana na wanawake watakaonufaika na mafunzo hayo ya siku 30 kutumia maarifa watakayopata ili kuwa mfano katika jamii kwa kuendeleza kilimo cha kisasa kitakachoongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, ameipongeza Serikali kwa kuifikisha programu hiyo katika halmashauri hiyo, akieleza kuwa itatoa fursa kwa vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Amewataka vijana kuchangamkia fursa hiyo na kuyatumia mafunzo watakayopata kuzalisha kwa tija, akisisitiza kuwa kilimo ni miongoni mwa sekta zenye fursa kubwa za ajira na kujipatia kipato.
Kwa upande wao, vijana na wanawake wanatarajiwa kunufaika na programu hiyo wameishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo, wakieleza kuwa mafunzo ya kilimo cha kisasa yatawasaidia kuongeza uelewa na kuachana na mbinu za kilimo cha kutegemea mvua ambazo, kwa mujibu wao, zimekuwa na matokeo yasiyoridhisha.
Kupitia programu hiyo, wanufaika wanatarajia kupata ujuzi na fursa ya kujenga msingi wa kilimo cha kibiashara, kuongeza uzalishaji na kujipatia kipato kupitia sekta ya kilimo.








Comments
Post a Comment