DODOMA: Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Nchini (TFSRP-P4R) imeanza kuleta matokeo chanya kwa wakulima wadogo nchini Tanzania, baada ya kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka wastani wa tani mbili hadi kufikia tani nane kwa ekari, kufuatia ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji.
Mafanikio hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa programu hiyo kilichofanyika katika Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), jijini Dodoma, chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Bw. Raymond Mndolwa.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau wa maendeleo wanaoshirikiana katika utekelezaji wa programu hiyo, wakiwemo wawakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA).
Kupitia programu hiyo, jumla ya skimu 84 za umwagiliaji nchini zimeingizwa katika mfumo rasmi wa usimamizi na matunzo shirikishi, unaowezesha wakulima wadogo kushiriki moja kwa moja katika kusimamia na kulinda miundombinu ya umwagiliaji kupitia Vyama vya Wamwagiliaji.
Hatua hiyo pia imeimarisha ukusanyaji wa ada za huduma za umwagiliaji na kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua, jambo linalochangia kuongeza uhakika wa uzalishaji wa chakula na kipato kwa kaya za wakulima.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, amewashukuru wadau wa maendeleo kwa mchango wao katika kufanikisha programu hiyo, huku akiahidi kuwa Tume itaendelea kusimamia viashiria vyote vya utekelezaji ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Amesema jitihada hizo zinalenga kukuza uchumi wa kaya za wakulima wadogo na kujenga uwezo wa sekta ya kilimo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa wadau na Msimamizi wa Mradi wa TFSRP kutoka Benki ya Dunia, Bw. Ernest Ruzindaa, ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa usimamizi wa utekelezaji wa programu hiyo.
Mafanikio hayo yanaonesha nafasi ya uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji katika kuongeza tija ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya wakulima wadogo nchini.














Comments
Post a Comment