Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga.
Wakala wa maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga wamesema kuwa wamejipanga kuhakikisha miradi yote iliyopo mkoani humo inayotoa huduma kwa wananchi haiathiriki na mvua zinazokuja hasa za Elniño ikiwa ni utekelezaji wa maagizo.
Haya yameelezwa na Meneja wa RUWASA mkoa wa Tanga Mhandisi Alkam Sabuni wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea hali ya utoaji huduma kwa wananchi ambapo amesema kuwa wamechukua hatua kuu tatu ambazo ni pamoja na kuzungushia ukuta katika visima ili kukinga mafuriko yasiweze kuchafua ubora wa maji au kuharibu miundombinu iliyotengenezwa.
Pamoja na hayo pia RUWASA imejipanga katika madawa ya kutibu maji kwenye yale maeneo ambayo wanadhani kutakuwa na ongezeko la tope katika maji wamejipanga vizuri na wana madawa ya kutosha kuweza kutibu maji, wametoa pia taarifa kwa wateja kuwa wahifadhi maji ya kutosha majumbani ili ikitokea kama athari zimekuwa kubwa wawe na maji ya kutosha.
Aidha amewataka wananchi kuwa wazalendo kulinda na kutunza miundombinu ya maji iliyopo ikiwa ni pamoja na kuwa mstari wa mbele kukemea uchafuzi wa mazingira na kukata miti ovyo hali ambayo inaweza kusababisha ukosefu wa huduma ya maji na kuathiri vyanzo vilivyopo.
"Niwaase sana wananchi wawe wazalendo wafahamu kwamba maji ni usalama wa nchi pale ambapo wanaharibu miundombinu na kuchafua maji tayari wanatishia usalama wa nchi na wanaisababishia Serikali hasara ya kutibu maji na wananchi , tunatumia gharama kubwa kujenga miundombinu iliyopo hivyo ni lazima ilindwe" amesisitiza Sabuni.
Meneja huyo ameongeza kuwa mkoani Tanga sasa ipo miradi mbalimbali inayotekelezwa ambayo inalenga kuboresha hali ya utoaji huduma na upatikanaji wa maji kwa wananchi ambapo jumla ya miradi 79 ikigharimu kiasi cha Shilingi Milioni 104 ambapo ipo katika hatua za utekelezaji ikitarajiwa kukamilika ifikapo June 2027.
Sabuni ameongeza kuwa mpaka sasa mkoani Tanga kuna vyombo (Sibiuso) 42 vilivyosajiliwa kisheria chini wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) ikiwa lengo lao ni kuhakikisha miradi yote iliyopo katika maeneo ya wananchi inalindwa na kuendelea kutoa huduma iliyokusudiwa na Serikali.
RUWASA Mkoa wa Tanga kwa sasa inahudumia watu zaidi ya Milion 2,400,000 , zaidi ya kaya 635,514 ambapo mpaka sasa katika hali ya utoaji wa huduma ya maji wamefikia asilimia 75 wakitarajia kufikia asilimia 85 baada ya kukamilika kwa miradi inayoendelea kitekelezwa.

Comments
Post a Comment