MKUU wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, ameipongeza Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MNUAT) kwa maendeleo makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho, akieleza kuwa uwekezaji huo umechangia kubadilisha taswira ya Wilaya ya Butiama na Mkoa wa Mara kwa ujumla.
Mtambi ametoa pongezi hizo leo, Novemba 17, 2026, alipompokea na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha MNUAT, Philemon Luhanjo, aliyefika mkoani Mara kwa ajili ya kushiriki kikao cha Baraza la Chuo.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Mtambi amesema chuo hicho kimepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake, hususan katika ujenzi wa miundombinu inayowezesha udahili wa wanafunzi katika Kampasi Kuu ya Butiama na Kampasi ya Tabora.
“Kuna maendeleo makubwa sana ambayo yamefikiwa na chuo, ikiwemo majengo ya Kampasi Kuu ambayo yamesaidia sana kubadilisha muonekano wa Butiama na Mkoa wa Mara kwa ujumla,” amesema Mtambi.
Amesema hatua nyingine muhimu ni kuanza kwa chuo hicho kutoa wahitimu wa programu mbalimbali mwaka huu, huku mahafali yake ya kwanza yakitarajiwa kufanyika Desemba 11, 2026, hatua inayoashiria kuendelea kukua kwa taasisi hiyo ya elimu ya juu.
Katika kuendeleza mafanikio hayo, Mtambi ameuhakikishia uongozi wa MNUAT kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na chuo hicho katika jitihada za kukiendeleza, ikiwemo kuwahamasisha wananchi wa Mara na wawekezaji wengine kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika Wilaya ya Butiama.
Aidha, amekitaka chuo hicho kuanza maandalizi ya kujenga uzio katika kampasi zake ili kuimarisha usalama wa maeneo ya chuo, kuweka mipaka inayoeleweka na kuzuia uwezekano wa kutokea kwa migogoro kati ya chuo na wananchi wanaokizunguka.
Kwa upande wake, Luhanjo amesema yupo mkoani Mara kwa ajili ya kushiriki kikao cha Baraza la Chuo, huku akieleza kuwa kesho wanatarajia kutembelea Kampasi ya Tabora kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika kampasi hiyo.
Katika ziara hiyo, Luhanjo ameambatana na Makamu Mkuu wa Chuo cha MNUAT, Profesa Lesakit Mellau.





Comments
Post a Comment