Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mhe. Mgore Miraji Kigera, akiwa katika ziara ya kikazi nchini Italia, ametembelea eneo la Balzona ambako ujenzi wa handaki (Tunnel) la reli unaendelea, ikiwa ni sehemu ya kujifunza teknolojia, ubunifu na mifumo ya kisasa inayotumika kuendeleza miundombinu ya reli.
Mradi huo, wenye thamani ya takribani Euro bilioni 11, ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya reli nchini Italia, huku Serikali ya Italia ikichangia asilimia 50 ya gharama za utekelezaji wake.
Ujenzi wa handaki hilo unalenga kurahisisha usafiri wa treni, kupunguza muda wa safari na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya reli kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi.
Ziara hiyo ina umuhimu wa kimkakati kwa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kujifunza teknolojia na kupata uzoefu wa nchi zilizoendelea katika uwekezaji wa reli. Pia, inaendana na dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuimarisha sekta ya reli kupitia uwekezaji wenye tija, teknolojia za kisasa na miundombinu itakayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuijenga Tanzania yenye mtandao imara wa usafiri wa reli, utakaorahisisha usafirishaji, kuchochea biashara, kuvutia uwekezaji na kuharakisha ukuaji wa uchumi, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Comments
Post a Comment