Akizungumza Novemba 6, 2026, katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mbunge huyo amesema jamii inapaswa kushirikiana kurejesha misingi ya malezi iliyoachwa nyuma, huku akitaka Serikali kupitia wizara zinazohusika kuchukua hatua kuhusu masuala ya ushoga na usagaji.
Amesema mjadala aliougusia katika Bunge hili ulikuwa mfupi, lakini amedhamiria kufungua mjadala mpana zaidi katika Bunge lijalo ili kujadili changamoto hizo na namna ya kukabiliana nazo.
Katika hatua nyingine, ameeleza kutounga mkono kufutwa kwa adhabu za viboko mashuleni, akipendekeza zirejeshwe kama sehemu ya kuimarisha nidhamu na malezi ya watoto.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kutambua umuhimu wa kuwalea watoto wa kiume na wa kike kwa usawa, akisema kwa muda mrefu jamii imekuwa ikiweka mkazo mkubwa katika malezi ya watoto wa kike na kuacha kuwapa uzito unaostahili watoto wa kiume.
Pia amewataka waandishi wa habari na wananchi kuwa waangalifu katika kusambaza picha za watu wanaohusishwa na ushoga, akidai kuwa kufanya hivyo kunaweza kuchangia kutangaza au kueneza maudhui hayo, badala ya kusaidia kukabiliana na changamoto anayoizungumzia.
Ikumbukwe kuwa malezi ya watoto ni jukumu la pamoja na kwamba jamii inapaswa kurejea katika misingi ya malezi na maadili, huku akiahidi kuendeleza mjadala huo katika Bunge lijalo Januari 26, 2027.

Comments
Post a Comment