Uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya nchi hiyo kueleza nia ya kutumia uzoefu huo katika kutekeleza mpango wa kujenga Mji wa Serikali katika mji mkuu wa Kinshasa.
Waziri Mkuu wa DRC, Mhe. Judith Suminwa Tuluka, amesema Tanzania imekuwa mfano muhimu wa kujifunza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, akibainisha kuwa ziara yake katika Mji wa Serikali Mtumba imempa fursa ya kuona kwa vitendo namna mradi huo ulivyotekelezwa na jinsi unavyoweza kuwa rejea katika mipango ya nchi yake.
Mhe. Judith ameyasema hayo leo, Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, mara baada ya kutembelea Mji wa Serikali Mtumba na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa DRC.
Amesema ziara hiyo ni sehemu ya kunufaika na ushirikiano uliopo kati ya mataifa hayo mawili, ambao umekuwa ukitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kuharakisha maendeleo.Aidha, ameushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini DRC kwa kuendelea kuimarisha uhusiano na nchi hiyo, akieleza kuwa hata baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, ubalozi huo ulikuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kumpongeza, jambo linalodhihirisha ukaribu na undugu uliopo kati ya mataifa hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Anjela Kairuki, amesema Tanzania inathamini ziara hiyo na inaendelea kutambua umuhimu wa uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza ushirikiano na DRC katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, kwa kutumia fursa na uwezo uliopo katika mataifa hayo ili kuleta manufaa kwa wananchi wake.
Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka ameambatana na ujumbe wake, ukiwemo Waziri wa Ujenzi wa DRC, Bwana John Banza Lunda.
Ziara hiyo inaendelea kuonesha umuhimu wa diplomasia ya ushirikiano katika kukuza maendeleo, ambapo uzoefu na mafanikio ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali yanakuwa fursa kwa mataifa mengine kujifunza na kuimarisha mipango yao ya maendeleo.




Comments
Post a Comment