KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha cheti cha kimataifa cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 kinatafsiriwa katika maboresho halisi ya utendaji, uwajibikaji na utoaji wa huduma zenye viwango kwa wananchi na wadau wa sekta ya bima nchini.
Amesema mafanikio ya kupata cheti hicho yanapaswa kuwa msingi wa kujenga utamaduni wa ubora unaozingatia ufanisi, uwazi, uwajibikaji na maboresho endelevu, badala ya kukifanya kuwa nyaraka ya kutunzwa ofisini bila kuleta mabadiliko yanayoonekana katika huduma zinazotolewa.
Dkt. Mwamba ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Cheti cha Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ISO 9001:2015 kwa TIRA, iliyofanyika katika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Bima House, Njedengwa jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa kupata cheti hicho si mwisho wa safari ya ubora, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya kuimarisha utendaji wa taasisi kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.
Amesema hatua hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya TIRA katika kuimarisha mifumo ya kiutendaji, kuzingatia taratibu na viwango vya ubora pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini.
“Cheti hiki kisiwe pambo la ofisi au nyaraka ya kutunzwa kwenye mafaili pekee, bali kiwe kielelezo cha utamaduni wetu wa kazi na dhamira yetu ya kutoa huduma bora kila siku,” amesisitiza Dkt. Mwamba.
Amefafanua kuwa matumizi sahihi ya mfumo huo yatawezesha kuimarisha michakato ya kazi, kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa majukumu, kuboresha utatuzi wa changamoto na kutumia maoni ya wadau kama nyenzo muhimu ya kutambua maeneo yanayohitaji maboresho katika utoaji wa huduma.
Aidha, amesema mafanikio hayo yanaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayoweka msisitizo katika mageuzi ya kitaasisi na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili kujenga taasisi zenye uwezo, ufanisi na zinazochangia maendeleo endelevu ya Taifa.
Akizungumzia nafasi ya sekta ya bima katika kukuza uchumi wa Taifa, Dkt. Mwamba ameipongeza TIRA kwa juhudi za kusimamia sekta hiyo, kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za bima na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa soko la bima nchini, akibainisha kuwa sekta hiyo ilichangia asilimia 2.11 ya Pato la Taifa mwaka 2025.
Katika kuendeleza mafanikio hayo, ameitaka TIRA kuhakikisha kampuni za bima nchini nazo zinajenga utamaduni wa kuwekeza katika mifumo ya usimamizi wa ubora ili kuongeza ushindani, kuimarisha imani ya wateja na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya kimataifa.
“Natoa rai kwenu kuendelea kuzihimiza kampuni za bima nchini kuwekeza katika mifumo ya usimamizi wa ubora ili kuimarisha ushindani, kuongeza uaminifu wa wateja na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyotambulika kimataifa,” amesema.
Vilevile, amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kutoa utaalamu, mwongozo na ushirikiano uliowezesha TIRA kufikia hatua hiyo, huku akilihimiza kuendelea kusaidia taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi kuimarisha mifumo yao ya usimamizi wa ubora.
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima nchini ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware, amesema Mamlaka hiyo inalenga kuhakikisha ofisi zake zote nchini zinafikia viwango vya Mfumo wa Usimamizi wa Ubora ifikapo mwaka 2028.
Amesema katika kutekeleza azma hiyo, TIRA itaendelea kuwekeza katika maboresho ya maeneo mbalimbali yanayochangia ubora wa huduma, yakiwemo miundombinu na majengo ya ofisi, kuongeza uwezo wa watumishi pamoja na kuboresha michakato ya kiutendaji inayotumika kuwahudumia wananchi na wadau wa sekta ya bima.
“TIRA itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha kuwa wadau wote, wakiwemo wananchi, Serikali, kampuni za bima, watumishi na watoa huduma, wanapata huduma zinazokidhi viwango vinavyotakiwa,” amesema Dkt. Saqware.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Abdallah Kileo, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, amesema kupatiwa cheti hicho kwa TIRA ni hatua muhimu inayoonesha dhamira ya Mamlaka hiyo katika kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyotambulika kimataifa.
Amesema uthibitisho huo unahusisha ofisi tano za TIRA, zikiwemo Makao Makuu ya Dodoma, Ofisi ya Zanzibar, Ofisi ya Dar es Salaam pamoja na Ofisi za Kanda ya Mashariki na maeneo mengine yaliyohusika katika utekelezaji wa mfumo huo.
Mhandisi Kileo ameeleza kuwa ISO 9001:2015 ni mfumo unaotoa mwongozo wa kusimamia ubora wa huduma kupitia taratibu madhubuti za kiutendaji, uwajibikaji na ufuatiliaji wa michakato, huku ukihimiza taasisi kuzingatia mahitaji ya wateja na kufanya maboresho endelevu.
Ameongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yana umuhimu mkubwa kwa TIRA kutokana na ukubwa wa majukumu yake, yakiwemo kutoa leseni kwa kampuni na wadau wa sekta ya bima, kusimamia ushindani wa haki, kulinda maslahi ya wateja, kudhibiti shughuli za bima na kusimamia biashara za bima zinazovuka mipaka ya nchi.
Amesema majukumu hayo yanahitaji mifumo imara ya usimamizi, uwajibikaji na uzingatiaji wa viwango vya kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha sekta ya bima inafanya kazi katika mazingira yenye ufanisi na kuaminika.
Ameeleza kuwa TBS itaendelea kutoa huduma za upimaji, uthibitishaji na tathmini ya mifumo ya usimamizi wa ubora kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza utamaduni wa ubora, kuongeza ufanisi na kuimarisha ushindani wa huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini.






Comments
Post a Comment