Katika ziara hiyo, Mbunge huyo amekabidhi mifuko mitano ya saruji, juzuu za kujifunzia pamoja na miswala ya kuswalia, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuchangia maendeleo ya taasisi za kidini na kuimarisha mahusiano baina ya waumini wa dini mbalimbali.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Sheikh Amani Kapama wa Msikiti wa Iringo, amempongeza Mheshimiwa Marwa kwa moyo wake wa kujitolea na utaratibu wake wa kutembelea na kusaidia taasisi za kidini, akisema hatua hiyo imekuwa daraja muhimu la kuunganisha jamii bila kujali tofauti za kiimani.
Amesema ushirikiano unaooneshwa na Mbunge huyo unachangia kujenga mshikamano baina ya Waislamu na wasio Waislamu, kuimarisha upendo na kuendeleza misingi ya umoja na amani nchini.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Agness Marwa amesema ataendelea kubuni na kutekeleza mipango mbalimbali ya kusaidia jamii, akieleza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kurejesha shukrani kwa jamii na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi ya kulitumikia taifa.
Amesisitiza kuwa hana budi kuendelea kujenga mahusiano mema na viongozi wa dini zote, kwa kuwa umoja, kuheshimiana na kushirikiana ni misingi muhimu ya kuijenga jamii yenye amani na maendeleo.
Ameongeza kuwa tofauti za imani hazipaswi kuwa sababu ya kutengana, bali zinapaswa kuwa fursa ya kuimarisha kuheshimiana, kusaidiana na kuishi kwa upendo.
Kupitia msaada huo, Mheshimiwa Marwa ameendelea kusisitiza umuhimu wa viongozi na waumini wa dini mbalimbali kushirikiana katika shughuli za kijamii na maendeleo, hatua inayosaidia kujenga jamii yenye mshikamano na utulivu.









Comments
Post a Comment