MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Mhe. Agnes Marwa, amehoji mpango wa Serikali wa kuanzisha kongani za viwanda wilayani Bunda na Jimbo la Musoma Mjini ili kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa huo.
Akiuliza swali hilo leo Novemba 4, 2026, Bungeni jijini Dodoma, Mhe. Agnes Marwa amesema Mkoa wa Mara una historia kubwa katika taifa kutokana na kuwa chimbuko la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, lakini bado unakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na viwanda vya kutosha.
Amesema serikali inampango Gani kupeleka kongani za viwanda katika mkoa wa Mara ikiwemo wilaya ya Bunda na Jimbo la Msoma Mjini.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha Mkoa wa Mara unakuwa na viwanda vya kutosha vitakavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali zinazopatikana mkoani humo na kutoa ajira kwa Watanzania.
Amesema Serikali imeelekeza halmashauri kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya miundombinu ya maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu na mashine za viwanda.
Aidha, amemtaka Mbunge huyo kusimamia matumizi ya fedha hizo ili ziweze kuchochea mapinduzi ya viwanda na kukuza uchumi katika maeneo ya pembezoni.

Comments
Post a Comment