SENGEREMA YAFIKIA ASILIMIA 97 YA UTOAJI WA CHAKULA KWA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI ZAFIKIA ASILIMIA 75
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imefikia asilimia 97 ya utekelezaji wa mpango wa utoaji wa chakula kwa shule za msingi 123, huku shule za sekondari 59 zikifikia asilimia 75 katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, hatua inayolenga kuimarisha afya, lishe na mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mafanikio hayo yamebainishwa katika kikao cha Kamati ya Lishe ya Wilaya ya Sengerema kilichofanyika kwa lengo la kupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli hizo, Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo, Bi. Neema Sappy, amesema mpango wa utoaji wa chakula shuleni unaendelea vizuri, huku mwitikio wa wazazi katika kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao ukiendelea kuridhisha.
Amesema ushiriki wa wazazi ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wanapokuwa shuleni, hivyo amewahimiza kuendelea kutimiza makubaliano yaliyofikiwa katika vikao vya kamati za shule na vijiji husika ili kuimarisha utekelezaji wa mpango huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya Wilaya, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Bw. Edward Maduhu, amewataka watendaji na wataalamu kutoka idara na vitengo mbalimbali kuongeza nguvu katika ufuatiliaji na usimamizi wa mpango wa utoaji wa chakula shuleni.
Bw. Maduhu amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhamasishaji kwa wananchi ili kuongeza ushiriki wao katika kuchangia chakula shuleni, akieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na jamii ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora.
Aidha, amewataka watendaji na wataalamu kuendelea kusimamia utekelezaji wa shughuli za lishe kwa karibu ili kuhakikisha juhudi zinazofanyika zinachangia kuboresha afya na ustawi wa watoto shuleni.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kimehimiza kuendelea kuadhimisha Siku ya Afya na Lishe katika kila kijiji, pamoja na kuishirikisha jamii kikamilifu katika kuhamasisha na kusimamia masuala ya afya na lishe.
Kupitia hatua hizo, Halmashauri inalenga kuimarisha uelewa na uwajibikaji wa jamii katika masuala ya lishe, kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni na kujenga mazingira yatakayowawezesha kujifunza wakiwa na afya bora.







Comments
Post a Comment