Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga.
Maboresho ya Bandari ya Tanga yaliyoghalimu zaidi ya Shilingi Bilioni 429.1 Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) imekuwa ni miongoni mwa wanufaika wakuu kupitia tawi lake lililopo mkoani hapa ambapo wananchi wanaotumia usafiri wa majini na shughuli za uvuvi wamekuwa wadau wao wakubwa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Benki ya watu wa Zanzibar tawi la Tanga Wahbi Ali alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa wafanyabishara waliopo kati ya Tanga na Zanzibar pamoja na wavuvi wanaotumia Majahazi wamekuwa wakiitumia benki hiyo kukopa kwaajili ya biashara zao.
Aidha Wahbi ameongeza kuwa muitikio kwa wanatanga ni mzuri tangu walipofungua tawi katika mkoa huu na hii imetokana na mahusiano ya karibu yaliyopo kati ya Tanga na Zanzibar.
"Tangu tumefungua huduma yetu katika mkoa wa Tanga muitikio umekuwa ni mzuri ukilinganisha na mahusiano ya ukaribu yaliyopo kati ya Tanga na Zanzibar muingiliano wa kibishara uliopo imetusaidia kuanza vizuri na Benki yetu inahudumia watu wote na tumejipanga kutoa huduma bora" amesema Wahbi.
Pamoja na hayo pia PBZ katika wiki hii ya huduma kwa wateja wamejipanga kukutana na wateja wake kwa lengo la kupokea maoni ili waweze kuboresha huduma zaidi.
Pia Benki hiyo imeanzisha mfumo wa kidigital ambapo mteja anaweza kupata huduma kwa haraka zaidi kupitia simu ya mkononi bila kwenda katika ofisi au tawi lolote kwaajili ya kufuata huduma.
"PBZ imeendelea kujiimarisha zaidi katika kutoa huduma bora kwa njia ya kidigitali kupitia huduma ya lipa hapa ambayo unaweza kufanya malipo yako kwa njia ya mtandao kwa gharama nafuu kupitia mitandao ya simu bila hata kwenda Benki" ameongeza Wahbi.
Mbali na hiyo PBZ inatarajia kuzindua rasmi huduma ya lipa Ada ikiwalenga wadau wa elimu kupitia taasisi mbalimbali ambapo wazazi na walezi wanaweza kufanya malipo ya ada kupitia mfumo huo huku mfumo ukihusisha na upatikanaji wa taarifa zote za kitaaluma pamoja na mahudhuriao ya wanafunzi.
PBZ imeendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi ambapo mpaka sasa imepungua matawi yake katika Mikoa ya Dar es salaam, Dodoma Mbeya , Tanga, Arusha na Morogoro ikitoa huduma za kibishara, mikopo kwa watumishi mbalimbali, wakulima ,wavuvi pamoja na wajasiriamali.



Comments
Post a Comment