Na. Wellu Mtaki, Geita
KAMPUNI ya GF Truck Equipment Smart imesema Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita yamefungua fursa kubwa ya biashara, baada ya kupata wateja wapya na kuuza zaidi ya magari 10 kwa wachimbaji na wadau mbalimbali wa sekta ya madini.
Kampuni hiyo imesema maonesho hayo yamekuwa na tija kwa biashara yake, huku baadhi ya wachimbaji wakifanya manunuzi ya magari na wengine kuonyesha nia ya kununua bidhaa na vifaa vinavyotolewa na kampuni hiyo.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa GF Truck Equipment Smart, Deus, amesema kampuni hiyo imepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wachimbaji, hali iliyochochea ongezeko la mauzo.
Amesema hadi sasa kampuni hiyo imekabidhi gari moja kwa mteja, huku ikiwa katika hatua za mwisho za kukabidhi mteja mwingine aliyenunua zaidi ya magari 10 kupitia maonesho hayo.
“Tunamshukuru Mungu kwa siku hii kwa sababu tumeweza kumkabidhi mteja wetu gari moja. Kupitia maonesho haya tumepata mzigo mkubwa wa mauzo, na kesho tunakwenda kumkabidhi mteja wetu mkubwa ambaye amechukua zaidi ya magari 10,” amesema.
Amesema mwitikio huo umeipa kampuni hiyo hamasa ya kuendelea kushiriki Maonesho ya Teknolojia ya Madini, kutokana na mahitaji makubwa ya magari na vifaa vinavyotumiwa katika shughuli za uchimbaji.
Deus amesema GF pia inachangia katika utekelezaji wa sera ya maudhui ya ndani kupitia kiwanda chake cha kuunganisha magari, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazopatikana nchini.
Amesema uwepo wa kiwanda hicho unalenga kukidhi mahitaji ya soko la ndani, sambamba na juhudi za Serikali za kukuza maudhui ya ndani katika sekta ya madini.
Aidha, ameipongeza Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Teknolojia ya Madini kwa kuendelea kuboresha maonesho hayo na kuyafanya kuwa jukwaa linalowakutanisha wachimbaji na watoa huduma mbalimbali.
“Tunawapongeza sana waandaaji wa maonesho haya kwa sababu kila mwaka tunapokuja tunapokelewa vizuri na tunaona uhitaji mkubwa kutoka kwa wachimbaji wanaohitaji magari na vifaa mbalimbali,” amesema.
Amesema GF pia imeungana na taasisi mbalimbali za fedha zinazoshiriki maonesho hayo, ambazo zimekuwa zikitoa huduma za kifedha kwa wateja na hivyo kusaidia kuchochea biashara.
Kwa upande wake, mmoja wa wateja wa GF aliyekabidhiwa gari katika maonesho hayo amesema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa wachimbaji wadogo na wadau wengine kwa kuwa yanawawezesha kupata bidhaa na huduma muhimu karibu na maeneo yao ya shughuli.
Amesema awali baadhi ya wachimbaji walilazimika kusafiri hadi viwandani kutafuta vifaa na mashine, lakini kupitia maonesho hayo wamepata fursa ya kuona, kulinganisha na kununua bidhaa hizo moja kwa moja.
Amesema ushirikiano wao na GF umekuwa ukiwasaidia kupata magari, vifaa na huduma zinazohitajika katika shughuli zao za uchimbaji.
Maonesho ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji, wazalishaji wa vifaa, taasisi za fedha na taasisi za Serikali, kwa lengo la kuonyesha teknolojia, bidhaa na fursa zinazopatikana katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
![]() |


Comments
Post a Comment