KATIKA kuendeleza shughuli mbalimbali za kuinua Mkoa wa Mara na kuimarisha ustawi wa jamii, Mbunge Agnes Marwa ametunukiwa Tuzo ya Heshima na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Mara, kwa kutambua mchango wake wa hali na mali katika kuimarisha Jumuiya hiyo na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.
Tuzo hiyo imekabidhiwa na Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Godfrey Kavenga, akiambatana na viongozi wa UWT, ambaye amesema hatua hiyo inalenga kutambua jitihada, kujitolea na ushirikiano wa Agnes Marwa katika kuendeleza shughuli za Jumuiya na kugusa maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali.
Kavenga amesema mchango wa Agnes Marwa umeonekana katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha Jumuiya ya UWT Mkoa wa Mara, huku akimtaka kuendelea na moyo huo wa kujitolea na kushirikiana na wanawake pamoja na jamii katika kuleta maendeleo.
Kabla ya kukabidhiwa tuzo hiyo katika hafla iliyofanyika kata ya MWISENGE Mh Agnes Marwa alifanya ziara na shughuli za kijamii katika Wilaya ya Rorya, ambako aliungana na Jumuiya ya Akina Mama Mkoa wa Mara chini ya Mwenyekiti wake, Nancy, kutembelea shule iliyokumbwa na janga la moto lililosababisha mabweni mawili kuteketea.
Ziara hiyo ililenga kuwapa faraja wanafunzi na walimu pamoja na kuonyesha mshikamano katika kipindi ambacho shule hiyo inaendelea kukabiliana na athari za tukio hilo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Agnes amesema shule hiyo si ngeni kwake, akieleza kuwa amekuwa akiitembelea na kushiriki katika shughuli zake mbalimbali, huku akibainisha kuwa hiyo ni mara yake ya tatu kufika shuleni hapo.
“Shule hii mimi si mgeni, leo ni mara yangu ya tatu kufika hapa. Nimefika kuungana nanyi katika hili na kuhakikisha tunaendelea kushirikiana,” amesema Agnes.
Katika hatua nyingine, Agnes amempongeza Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, kwa kazi mbalimbali anazozifanya katika jimbo hilo, akisisitiza umuhimu wa viongozi kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto na kusukuma mbele maendeleo.
Akizungumza na wanafunzi hao, Agnes amewataka kutumia elimu kama msingi wa kujenga maisha yao na kufikia ndoto zao, huku akiwataka kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwatoa kwenye mstari wa mafanikio.
Amesema kupitia programu yake ya Ondoa Zero, yuko tayari kutoa motisha kwa wanafunzi watano watakaofanya vizuri katika mtihani ujao wa taifa, sambamba na kuendelea kuwahamasisha walimu katika juhudi za kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, amewataka vijana kuheshimu elimu, kuzingatia maadili na kufanya maamuzi yenye kulinda mustakabali wao, akisisitiza kuwa tamaa na vishawishi vinaweza kuwafanya wapoteze mwelekeo wa maisha.
Kwa vijana wa kiume, amewataka kuwa makini na kulinda usalama na heshima ya miili yao, huku akisisitiza umuhimu wa kukataa vishawishi na vitendo vinavyoweza kuwaathiri katika maisha yao ya baadaye.
Tuzo hiyo pamoja na shughuli alizofanya Rorya ni sehemu ya matukio yanayoonyesha namna Agnes Marwa anavyoendelea kushiriki katika shughuli za kijamii, elimu na uimarishaji wa Jumuiya katika Mkoa wa Mara.




Comments
Post a Comment