Watanzania wametakiwa kuanza kutumia nishati safi na rafiki ya Briquettes, baada ya kubainika kuwa ni nafuu, inadumu kwa muda mrefu na ni rafiki kwa mazingira.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kisome Enterprises, Elias Kisome, mara baada ya kutembelea banda la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Kisome amesema kupitia elimu aliyoipata bandani hapo, imebainika kuwa Watanzania wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu faida za matumizi ya nishati safi kwa kupikia.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa wataalamu wa STAMICO, tani moja ya makaa ya mawe inauzwa kati ya Shilingi laki nane hadi milioni moja na inaweza kutumika kwa muda mrefu, hivyo kumuwezesha mwananchi kuokoa gharama za kununua mkaa wa miti mara kwa mara.
"Nimejifunza kitu kikubwa hapa. Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania hususan wa vijijini kuelimishwa kuhusu nishati hii mbadala," alisema Kisome.
Aidha, amesema tofauti na mkaa wa miti unaochangia uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti ovyo, matumizi ya nishati safi ni endelevu na salama na yanapaswa kuhamasishwa kwa jamii.
Sambamba na hilo, wananchi wametakiwa kujiandaa mapema kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa, kwa kuweka akiba ya nishati hiyo pamoja na kuchukua tahadhari kwa kuhama katika maeneo ya mabondeni na maeneo hatarishi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.


Comments
Post a Comment