Tanzania na Misri zimejadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya ulinzi na teknolojia za anga, ikiwemo kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia kwa manufaa ya pande zote.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Uzalishaji wa Kijeshi na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Luteni Jenerali Ashraf Salem Zaher, jijini El Alamein, Misri.
Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 10, Septemba 2026, wakati Tanzania ikishiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Anga na Teknolojia za Anga za Juu ya El Alamein (ELIAS).
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili fursa za kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Misri katika maeneo ya ulinzi na teknolojia za anga, pamoja na umuhimu wa kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya ELIAS unalenga pia kujenga na kuimarisha mahusiano ya kimkakati na wadau wa kimataifa, hususan katika sekta za ulinzi, anga na teknolojia za kisasa, kwa kuzingatia maslahi ya pamoja na fursa za maendeleo ya kiteknolojia.
Maonesho hayo yanaendelea kutoa fursa kwa Tanzania kujifunza na kubadilishana uzoefu na mataifa mbalimbali pamoja na wadau wa kimataifa katika sekta ya anga na teknolojia za juu.






Comments
Post a Comment