Na Angela Sebastian
Bukoba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekabidhi mashine mbili za kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Bukoba, ikiwa ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo kusaidia kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga.
Mashine hizo zimekabidhiwa Septemba 9, 2026, na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Neema Mwakalyelye, katika hafla fupi iliyofanyika hospitalini hapo.
Mwakalyelye amesema mashine hizo ni ya kutunza joto la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito pungufu, pamoja na mashine ya kuwasaidia watoto wenye homa ya manjano kupona.
Amesema mpango huo umetokana na mchango wa hiari wa watumishi wa TAKUKURU, ambao wamejichanga na tayari wamefikisha vifaa hivyo katika mikoa 25 kati ya 28 inayolengwa Tanzania Bara.
Kwa mujibu wake, jumla ya mashine 56 zimekwishatolewa, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo ili hospitali za rufaa ziwe na vifaa vya kutosha.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dk.
Sophia Mosha, amesema hospitali hiyo hupokea kati ya watoto wachanga wagonjwa 790 hadi 930 kwa mwaka, wakiwemo waliozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito mdogo, ambao wengi huhitaji huduma maalumu za uangalizi.
Dk. Mosha amesema kuanzishwa kwa kitengo cha huduma kwa watoto hao kumeongeza ubora wa huduma na kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.
Hata hivyo, amesema kitengo hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa jengo pamoja na upungufu wa vifaa tiba.
Ameeleza kuwa hospitali inahitaji mashine 30 za kusaidia watoto wachanga kupumua, lakini kwa sasa ina mashine 10 pekee, hivyo kuna upungufu wa mashine 20. Pia, zinahitajika mashine 10 za kutibu watoto wenye homa ya manjano, huku zilizopo zikiwa nne pekee, ikiwa ni upungufu wa mashine sita.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amepongeza TAKUKURU kwa hatua hiyo na kuahidi kutumia nafasi yake kuhamasisha watumishi pamoja na wageni wanaofika ofisini kwake kutoka ndani na nje ya nchi kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali za mkoa huo.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Issaya Tendega, amewashukuru watumishi wa TAKUKURU kwa kujitoa na kuchangia vifaa hivyo, akisema bajeti ya Serikali haiwezi kukidhi mahitaji yote ya wananchi kwa wakati mmoja.
Amewataka taasisi za Serikali na binafsi kujitathmini na kuandaa mikakati ya kuunga mkono juhudi hizo, ili hospitali ziweze kupata mashine na vifaa vingine muhimu vya kuokoa maisha ya watoto wachanga.





Comments
Post a Comment