Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amepongeza maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Watunza Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), akieleza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha chama hicho na kuendeleza tasnia ya kumbukumbu na nyaraka nchini.
Kikwete ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya maandalizi ya Mkutano Mkuu huo kutoka kwa Mwenyekiti wa TRAMPA, Devotha Mrope, aliyefika ofisini kwake Mtumba, Dodoma pamoja na Kamati Tendaji ya chama hicho.
Amesema ameridhishwa na maandalizi yaliyofanyika, huku akiwapongeza viongozi wa TRAMPA kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwatakia maandalizi mema kuelekea mkutano huo.
“Tumewapongeza kwa kazi nzuri ya maandalizi na tunatarajia mkutano mzuri unaolenga kuimarisha chama chao na tasnia yao,” amesema Kikwete.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili na kuweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha TRAMPA pamoja na kuendeleza taaluma na tasnia ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini.


Comments
Post a Comment