MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema Serikali ya Mkoa imetenga kifuta jasho cha Shilingi 500,000 kwa kila mmoja wa wafanyabiashara 44 walioathirika na moto ulioteketeza sehemu ya Soko la Machinga Complex jijini Dodoma.
Senyamule ameyasema hayo leo Septemba 21, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, akieleza kuwa fedha hizo zitatolewa kama faraja kwa wafanyabiashara hao wakati wakisubiri kurejea katika maeneo yao ya biashara.
Amesema kifuta jasho hicho hakilengi kufidia thamani ya mali walizopoteza, bali ni hatua ya kuwapa faraja na kuwasaidia katika kipindi cha kusubiri kurejea kwenye shughuli zao za biashara.
“kifuta jasho si jambo linalingana na gharama uliyopoteza. Kifuta jasho ni kitu cha kukupa faraja. Kwa hiyo, kila mmoja kati ya watu 44 atapewa Shilingi 500,000 ili angalau aweze kupata kifuta jasho wakati anasubiri siku 10 za kurudi kwenye mazingira yake ya biashara,” amesema Senyamule.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu mazingira ya biashara ili kuhakikisha matukio kama hayo hayajitokezi na kurudisha nyuma juhudi za wananchi.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara kufuata taratibu za usalama zinazowekwa na wataalamu, ikiwemo kuhakikisha wanazima taa na soketi zote wanapomaliza shughuli zao za biashara.
Senyamule amesema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza uwezekano wa kutokea kwa hitilafu zinazoweza kusababisha taharuki na majanga ya moto, akibainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiacha taa zikiwa zimewashwa baada ya kumaliza shughuli zao.
Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za usimamizi na ufuatiliaji ili kulinda shughuli na mali za wananchi dhidi ya majanga yanayoweza kuzuilika.




Comments
Post a Comment