NMB YAPANUA FURSA ZA FEDHA KWA WACHIMBAJI WADOGO , YATOA MIKOPO HADI ASILIMIA 100 YA VIFAA VYA UCHIMBAJI.
Na. Wellu Mtaki,Dodoma
Benki ya NMB imeendelea kuweka msisitizo katika kuwawezesha wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wanaotoa huduma kwenye migodi kwa kuwapatia mikopo, elimu ya fedha pamoja na ushauri wa kibiashara, hatua inayolenga kuongeza uwezo wao wa kukuza shughuli zao.
Akizungumza kuhusu huduma hizo, Deogratius Shirima kutoka Idara ya Biashara ya NMB Makao Makuu, amesema benki hiyo ina dawati maalum linaloshughulikia biashara na huduma mbalimbali zinazowalenga wateja wanaofanya shughuli katika sekta ya migodi.
Shirima amesema NMB imekuwa ikitoa mikopo kwa wachimbaji wadogo kwa masharti na riba nafuu, huku ikiambatanisha huduma hizo na elimu kuhusu mazingira, fedha na masuala ya ardhi.
“Kwa wachimbaji wadogo tunatoa mikopo yetu kwa riba nafuu Lakini pia tunatoa elimu ya mazingira, elimu ya fedha na elimu ya ardhi, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali,” amesema Shirima.
Ameongeza kuwa NMB pia inaangalia namna ya kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma mbalimbali katika maeneo ya migodi.
Kwa baadhi ya mikopo ya vifaa vya kazi, vifaa hivyo vinaweza kutumika kama dhamana, na mteja anaweza kupata fedha kulingana na thamani ya kifaa pamoja na vigezo vingine vinavyotumiwa na benki.
Kwa mujibu wa Shirima, NMB pia huzingatia mambo mbalimbali kabla ya kutoa mikopo, ikiwemo kumbukumbu za kibenki za mteja, utunzaji wa mazingira na uwezo wa biashara husika huduma kwa wafanyabiashara na sekta ya migodi
Shirima amesema upande wa Commercial wa NMB unaendelea kuhudumia kampuni na wafanyabiashara wanaojihusisha na shughuli mbalimbali katika sekta ya migodi.
Amesema hadi kufikia mwezi Juni, biashara zinazohusiana na sekta hiyo zilikuwa zimefikia thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 350, huku akieleza kuwa shughuli hizo zinaendelea kukua.
Mbali na mikopo, NMB imekuwa ikitoa huduma za ushauri wa biashara na elimu ya fedha kupitia programu na majukwaa mbalimbali, ikiwemo NMB Business Club, kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kuelewa namna bora ya kusimamia fedha na kukuza biashara zao.
Aidha Shirima ameeleza kuwa NMB imezindua mfumo wa kadi unaolenga kuwawezesha wateja kupata fedha kwa mahitaji ya muda mfupi ya biashara na kupitia mfumo huo, mteja anaweza kupata mkopo wa hadi Shilingi milioni 50, ambapo iwapo mkopo utatumika na kurejeshwa ndani ya siku tano, mteja hatatozwa gharama ya riba kwa utaratibu uliowekwa na benki.
Amesema huduma hiyo inalenga kuwapa wafanyabiashara unafuu katika kukabiliana na mahitaji ya kifedha ya muda mfupi na kuendelea na shughuli zao bila usumbufu.
pia amewataka wafanyabiashara, wakiwemo wachimbaji wadogo na wale wanaotoa huduma katika migodi, kutumia fursa zinazotolewa na NMB ili kukuza biashara zao.


Comments
Post a Comment