Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Musoma(MUWASA) Esther Gilyoma amesema kuwa changamoto iliyojitokeza ya maji na kusababisha mgao Manispaa ya Musoma na maeneo yanayohidumiwa na Mamlaka yatatuliwa.
Ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za mamlaka hiyo ambapo ameweza kufafanua hali ilivyokuwa huku akiwaomba radhi wateja wote wanaohudumiwa na Mamlaka hiyo kwa kupitia changamoto hiyo.
Gilyoma amefafanua kuwa mara baada ya kujitokeza kwa changamoto hiyo na wataalam kubaini chanzo mamlaka ilihakikisha inatafuta ufumbuzi wa haraka na jitihada zilianza kuchukuliwa ambapo taarifa iliwasilishwa Wizara ya maji.
Jitihada madhubuti za Wizara ya maji ambayo ndie mlezi wa Mamlaka za maji chini ya Waziri mahili Jumaa Aweso zimeweza kuondoa adha hiyo ya maji kwa kuhakikisha huduma inaimarika kama ilivyokuwa hapo awali.
Hatua hizo za makusudi zilichukuliwa na MUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya maji na zimewezesha kupata Kifaa cha kudhibiti kasi kwa kubadilisha marudio (VFD) kutoka mradi wa maji wa Same-Mwanga ambacho kiliwasili Septemba 3,2026 na kazi ya matengenezo imeanza.
Mzabuni aliagiza kifaa Nchini China na kiliweza kuwasili na kufungwa na kufanyiwa majaribio mnamo Septemba 21,2026 na wataalam kutoka Wizara ya maji,Mzabuni na MUWASA.
" Kuharibika kwa kifaa hicho kilichangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa upungufu wa maji kwenye maeneo mengi yaliyopo kwenye miinuko hali iliyolazimu MUWASA kutoa huduma ya maji kwa mgao ili kupunguza adha ya ukosefu wa maji maeneo ya zaidi ya mitaa 16,"amesema Gilyoma.
Ametaja baadhi ya mitaa iliyopatwa na changamoto ya upungufu wa maji kuwa ni pamoja na Zanziba,Mgaranjabo,Buhare,Matawi ya juu, Kurumuli,Etaro,Kiara,Kwangwa,Chagangala,Nyabisare,Rwamlimi,Songe,Bweri,Morembe,Nyabange,Mtakuja,na Songambele.
Hakusita kutoa pongezi na shukrani kwa viongozi wa Wizara kwa ushauri na maagizo yao ambayo yameweza kufanikisha kutatua changamoto hiyo watumishi wa MUWASA wanaushukuru uongozi kwa ushirikiano huo.
Aidha Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kuleta mitambo ya uzalishaji ya kusukuma maji katika eneo la Bukanga pia Wizara ya maji imeweka zaidi ya billion 30 huu ni uwekezaji mkubwa na hakuna mradi wa maji unaoweza kufanyika pasipokuwa na rasilimali fedha.
Mamlaka ya maji imejipanga kutoa huduma kwa wateja na ipo kwa ajili ya utekelezaji wa kutoa huduma kwa wananchi na kuendelea kupata maji safi na salama.
Amewakumbusha wateja na wananchi wote kutunza miundombinu ya maji pia kutoa taarifa ya uharibifu wa miundombinu ikiwemo mivujo ya maji.
Hivi sasa uzalishaji umeongezeka na kufikia lita million kwa siku 32 za ujazo tofauti na wakati wa hali ya upungufu wa maji uzalishaji ulipungua hadi lita million 22 kwa siku.
Nao Asia Stephano mkazi wa Buhare Nyamambara mkazi wa Songambele bondeni na Baraka Mwita wa Matawi ya juu wameipongeza MUWASA kwa kutoa taarifa na ratiba ya hali ya upungufu wa maji na namna mgao ulivyotolewa kwa maeneo yaliyopata adha hiyo wamepongeza huduma kurejea hivi sasa maji yanapatikana muda wote.





Comments
Post a Comment