WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kufanya vizuri katika utoaji wa huduma na kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa huduma bora za uhamiaji barani Afrika.
Katambi amesema hayo leo, Septemba 6, 2026, akizungumza katika kikao cha viongozi waandamizi wa Idara ya Uhamiaji, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na wageni wanaoingia nchini.
Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa pasipoti, akieleza kuwa pasipoti ya Tanzania imekuwa miongoni mwa pasipoti bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiwa na mifumo imara ya kiusalama inayoweza kuwa mfano kwa nchi nyingine.
“Ni jambo kubwa ambalo Watanzania wanapaswa kujivunia kwamba pasipoti yetu ni nzuri na ina security features ambazo kwa nchi nyingine ni ya mfano,” amesema Katambi.
Aidha, Katambi ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kutambuliwa kutokana na ubora wa huduma zake, akisema hatua hiyo ni ushahidi wa weledi, matumizi ya teknolojia na kujituma kwa watumishi wa idara hiyo.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi na maelekezo yanayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kutabasamu.
Katika hatua nyingine, Waziri Katambi amewataka viongozi na watumishi wa Uhamiaji kuendelea kuzingatia sheria na taratibu, kufanya uhakiki wa kina wa waombaji wa huduma, kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na kupambana na rushwa, udanganyifu na vitendo vya kihalifu.
Amesisitiza pia umuhimu wa kulinda siri na taarifa za wananchi, akieleza kuwa taarifa zinazokusanywa na Idara ya Uhamiaji ni sehemu ya taarifa muhimu za taifa na zinapaswa kulindwa dhidi ya kufika katika mikono isiyo salama.
Katambi ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Idara ya Uhamiaji na taasisi nyingine za ulinzi na usalama, pamoja na wananchi, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda nchi na wakati huo huo kuhakikisha huduma za uhamiaji zinazohusiana na utalii, biashara na masuala ya kidiplomasia zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.
Amesema Idara ya Uhamiaji inapaswa kuongeza elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, hususan redio na televisheni, ili kuwawezesha wananchi kuelewa taratibu zinazohusiana na pasipoti, visa, uraia na huduma nyingine za uhamiaji.
“Masuala ya uhamiaji na uraia ni mambo ambayo yana taratibu zake, hivyo ni muhimu wananchi kuelimishwa ili waelewe vizuri,” amesema.
Waziri Katambi pia amesisitiza uwajibikaji, ufuatiliaji, usawa na haki kwa waombaji wa huduma, akiwataka viongozi kuhakikisha maagizo yanayotolewa yanafuatiliwa hadi utekelezaji wake kukamilika.
Amesema utoaji wa huduma bora ni sehemu ya kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona wananchi wanapata huduma zinazowafanya watabasamu.
Katambi amesema tayari ameona maboresho mbalimbali katika huduma za Uhamiaji, ikiwemo katika viwanja vya ndege vya Zanzibar na Dar es Salaam, ambako ameona kuongezwa kwa madawati ya huduma na maeneo ya kuchanganua pasipoti ili kupunguza muda wa wananchi na wageni wanapohudumiwa.
Ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa hatua hizo, akisema uboreshaji wa huduma, matumizi ya teknolojia na weledi wa watumishi ni msingi muhimu wa kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa huduma za uhamiaji barani Afrika.
Sambamba na hayo Waziri Katambi amesema pasi ya kusafiria inayotolewa na Idara ya Uhamiaji imeshinda tuzo ya kuwa Pasi bora katika Ukanda wa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika.
"Pasi ya kusafiria ya Tanzania ina alama za usalama ambazo kwa nchi nyingine ni ya mfano huku matumizi ya teknolojia na utoaji wa huduma Bora za Kiuhamiaji yakizidi kuipa sifa Idara ya Uhamiaji kwa Afrika nzima na kuifanya Idara hiyo kupokea tuzo ya Huduma Bora iliyotolewa tarehe Mosi mwezi wa nane nchini Ghana". Amesema
Kikao cha Makamishna na Maofisa wanaoshughulikia Masuala ya Uraia na Vibali vya Ukaazi kimefanyika Ofisi za Uhamiaji Kurasini,jijini Dar es Salaam.










Comments
Post a Comment