TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la taasisi zinazofanya vizuri katika kuboresha huduma na kutoa huduma bora kwa jamii, katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali (CEO Forum 2026).
Ushindi huo umetangazwa leo, Septemba 29, 2026, wakati wa kikao hicho kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), huku JKCI ikitambuliwa kwa hatua zake katika matumizi ya huduma za kidijitali, kuongeza kiwango cha kuridhika kwa wateja na ukuaji wa idadi ya wateja katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Tuzo hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ikiwa ni sehemu ya kutambua taasisi zilizofanya vizuri katika kuboresha huduma na kuongeza thamani kwa jamii.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema ushindi huo ni matokeo ya juhudi za pamoja za watumishi wa taasisi hiyo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zinazotumia teknolojia na kukidhi mahitaji yao.
“Tuzo hii ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na watumishi wa JKCI kwa moyo, nidhamu na kujitolea. Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za kila mmoja wetu na nguvu ya timu yetu,” amesema Dkt. Kisenge.
Amesema tuzo hiyo ni chachu kwa JKCI kuendelea kuweka viwango vya juu katika utoaji wa huduma, kuwahudumia wananchi na wadau kwa uadilifu na kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa mfano wa ubora katika utoaji wa huduma nchini.
Kwa ushindi huo, JKCI imeendelea kujenga taswira ya taasisi inayoweka mkazo katika ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia na kuridhisha mahitaji ya wananchi.


Comments
Post a Comment