Amani na Maendeleo Organization ( AMO) yaiomba jamii kudumisha amani kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo kwa Taifa lolote.
Akitoa ujumbe huo kwa niaba ya Shirika Katibu Mkuu Mtendaji Jovina John Massano amesema Taifa lolote lisilokuwa na amani maendeleo huwa hafifu ieleweke kuwa Ushirikiano,Umoja,Uwajibikaji na Upendo ndio chanzo cha amani katika Taifa lolote Duniani na ndio msingi wa maendeleo.
"Sisi ni wadau wa amani tunawaomba wadau, Vijana, taasisi za dini, viongozi wa Mila na desturi, viongozi wa Serikali,wazee,vyama vya siasa,wanaharakati na jamii yote kuishi na kuenzi amani tulioachiwa na waasisi wa Taifa letu wakiongozwa na Hayati Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kusikilizana na kushirikiana".
Tarehe 21 Septemba 2026 huazimisha siku ya amani kimataifa mwaka huu imejikita kuwekeza katika Amani na tunatambua pamoja kuamini kuwa Amani ni zaidi ya kutokuwepo kwa vita.
Pia Amani inahusiana na usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu, fursa sawa ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni muhimu katika kushughulikia changamoto zinazoikabili jamii.
AMO inaamini haya maadhimisho yanatoa kipaumbele maalum kwa wajenzi wa amani wa kila siku wanaohamasisha hatua za kijamii kwa kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuchangia katika amani.
Siku ya Amani Kimataifa ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1981 na kutengwa tangu mwaka 2001 kama kipindi cha kujitolea kwa kutotumia nguvu na hivyo kusitisha mapigano.
Kaulimbiu ya mwaka 2026 ni “Wekeza katika Amani: Kwa Kila Mtu, Kila Mahali, Kila Siku” kauli hii inatoa wito kwa watu binafsi,taasisi na jamii kutambua amani kama jukumu la pamoja na kuchangia katika kuiendeleza katika maisha ya kila siku.
AMO inatambua mshikamano wa kijamii na kuchangia katika kujenga amani ya kudumu kuanzia ngazi ya chini kabisa Amani haipatikani tu kupitia katika majadiliano au makubaliano ya kisiasa bali Amani ya kweli inajengwa na moyo wa uzalendo pia madarasani, mitaani na katika jamii popote ambapo watu hukutana kwa uwazi, katika mazungumzo na kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu.
Kwa muktadha huu, kuendeleza amani kunahusiana kwa karibu na kulinda haki msingi za binadamu, usawa, utu sanjari na kukomesha kabisa sera za kibaguzi.
AMO inatambua namna Umoja wa Mataifa unavyokazia umuhimu wa kujenga na kudumisha amani ambapo kuliwezesha kuanzishwa kwa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kujenga Amani mwaka 2005 ikishirikiana na Ofisi ya Kusaidia Ujenzi wa Amani pamoja na Mfuko wa Kujenga Amani.
Tume hiyo inaunga mkono juhudi zinazolenga kuzuia na kutatua migogoro, pamoja na kukuza haki, maridhiano, haki msingi za binadamu na usawa wa kijinsia.
Siku hii ya Amani Kimataifa kwa mwaka 2026 inatoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua madhubuti za kuunga mkono amani kuwasaidia wengine, kutetea mabadiliko chanya,kuandaa mazingira ya majadiliano sambamba na kutumia majukwaa ya mawasiliano kueneza ujumbe wa amani na matumaini.
Hatua hizi huchangia katika juhudi pana zaidi za kujenga jamii zenye
kuimarishana na kupelekea kujenga utamaduni wa amani ambapo kunahitaji ushiriki wa kila mtu popote pale alipo na kwamba huu ni mchakato wa kila siku.
Tunashuhudia wanaharakati, viongozi wa asasi za kiraia, walinda amani na wapatanishi wameendelea kuwa nguvu muhimu katika kuunganisha jamii zilizogawanyika kutokana na migogoro.
Katika maadhimisho hayo huambatana na tukio la igongaji kengele ya amani zoezi linalofanyika katika bustani za makao makuu ya umoja wa Mataifa.
Hivi sasa tunashuhudia ongezeko la migogoro,vurugu na migawanyiko katika sehemu nyingi duniani na njia mojawapo ya kujenga amani ya kudumu ni kuwekeza katika maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.
Wito kwa Jamii iwekeze katika elimu, afya na maendeleo kwa watu wote ,Vijana wanapaswa kutambua umuhimu wa amani wasiwe tayari kujihusisha na vitendo vinavyoelekea kuvuruga Amani.
Amani ikitoweka hakuna atakayekuwa salama kila mmoja atakuwa mhanga wa ukosefu wa amani kushiriki,kushawishi na kuhamasisha vurugu zinazopelekea watu kuteseka na kuishi kwa kuhamahama
Pia viongozi wanapaswa kuelekeza rasilimali zaidi katika sekta muhimu zinazogusa maisha ya wananchi ya kila siku kwa maana ya afya,elimu, lishe na mifumo ya ulinzi wa kijamii kwani maendeleo ya kijamii na kiuchumi husaidia kupunguza mazingira yanayochochea migogoro inayopelekea kutokuaminiana miongoni mwa wananchi.
Amani ya kweli haiwezi kupatikana bila kuwepo kwa taasisi imara zinazoheshimika na kuaminika sasa basi ni muhimu kujenga taasisi na mifumo ambayo watu wanaweza kuiamini.
Amani na Maendeleo Organization (AMO), inajenga Jamii kwa kuhamasisha Amani na kuchochea Maendeleo katika nyanja zote kwa kuielimisha jamii kwa ustawi wa wote na Taifa kwa ujumla. _*_Amani ni nguzo yetu tuilinde_*


Comments
Post a Comment