*Asema lengo ukuaji ufikie asilimia saba ifikapo mwaka 2030*
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema CCM inalenga kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia saba ifikapo mwaka 2030, huku ukichochea ongezeko la kipato na kuboresha maisha ya wananchi.
Wasira amesema hayo leo (Agosti 21,2026) wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM mkoani Singida, akieleza kuwa ukuaji wa uchumi hautakuwa na maana iwapo hautaonekana katika maisha ya mtu mmoja mmoja kupitia ongezeko la kipato na fursa za kiuchumi.
Amesema katika Ilani ya CCM, chama hicho kimeweka msisitizo wa kukuza uchumi jumuishi unaolenga kumwezesha kila Mtanzania kunufaika na ukuaji wa uchumi.
“Katika Ilani yetu tumesema tunataka uchumi mkuu ambao kila siku mnasikia Tanzania uchumi wako unakuwa kwa asilimia 6.3. Lakini hii haitoshi. Tunataka uchumi huu usaidie maisha ya mtu mmoja mmoja,” amesema Wasira.
Ameeleza kuwa CCM inalenga kuona mapato ya wananchi yanaongezeka, huku akitolea mfano wakulima wa alizeti mkoani Singida ambao, kwa mujibu wake, wana nafasi kubwa ya kuongeza kipato kupitia kilimo na uwekezaji katika viwanda vya kuchakata zao hilo.
Wasira amesema Serikali imeweka hatua mbalimbali, ikiwamo kuongeza kodi kwa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje, kwa lengo la kuwahamasisha wakulima wa alizeti kuongeza uzalishaji na hivyo kuongeza mapato.
Amesema hatua hiyo pia inalenga kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kusindika alizeti, ambavyo vitaongeza thamani ya zao hilo na kutoa ajira kwa wananchi.











Comments
Post a Comment