Na Mwandishi wetu Jovina Massano ;Musoma.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mara imeeleza kuwa waandishi wa habari na jamii ni wadau muhimu katika kuibua mianya ya rushwa.
Hayo yamesemwa katika mafunzo ya siku moja ya TAKUKURU na kazi zake na Majukumu yake yenye lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kupata uelewa mpana wa namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
TAKUKURU inatambua umuhimu wa Waandishi wa habari kuwa ni miongoni mwa wadau muhimu wa utoaji elimu ya rushwa kwa jamii.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mara Sadiki Nombo amesema waandishi wa habari na jamii ni wadau muhimu wa kuibua mianya ya rushwa hapa nchini.
Aidha Nombo amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo na warsha mbalimbali kwa wadau wakiwemo waandishi wa habari ili kuowaongezea uelewa wa kutosha kuhusiana na majukumu na mapambano ya TAKUKURU dhidi ya rushwa.
TAKUKURU katika majukumu yake na kazi zake hutoa elimu kwa Umma hivyo amewaomba waandishi wa habari kutoa habari kwa uwazi na ukweli wakati wa kutoa taarifa zao.
Kwa kuwa waandishi wa habari wanauwezo na nafasi kubwa ya kuwafikia wananchi na kuwapa elimu kuhusiana na umuhimu wa kutoa taarifa mapema ya viashiria sambamba na madhara ya rushwa.
"TAKUKURU hufuatilia matumizi mabaya ya ofisi za Serikali kwa maslahi binafsi,pia hufanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa na kufuatilia matumizi ya fedha za umma na kufanya uchambuzi wa mifumo na kuzuia mianya inayoweza kuchochea rushwa," amesema Nombo.
Hata hivyo amewataka waandishi wa habari na jamii kutoa taarifa za uwepo wa mianya ya rushwa hasa katika fedha zinazotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo zinazotolewa na Serikali.
Eunice Kiwia afisa wa TAKUKURU amewaomba waandishi wa habari kutoa habari za kweli na uwazi ili wananchi wapate taarifa sahihi pia amewaasa na kutoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kutoa hongo pindi wanaohitaji huduma na kuwaelekeza kufuata utaratibu wa malipo ili kujiepusha na vitendo vitakavyosadikiwa ni rushwa.
Akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari Afisa uchunguzi TAKUKURU na mkuu wa dawati la uzuiaji rushwa Celestine Mayunga amesema katika miradi hufuatilia fedha na kudhibiti.
Ametoa ufafanuzi wa kuhusu mifumo na hufuatilia matumizi ya fedha katika miradi na pia hufanya chambuzi za mifumo ya fedha ikibainika kama kuna ucheleshwaji wa miradi ya maendeleo.
Ameweza kutoa mojawapo ya fedha kiasi cha Tsh. Millioni 38.5 iliyookolewa katika mradi wa barabara ya majita road mara baada ya mkandarasi kuziba mashimo chini ya kiwango hivyo TAKUKURU ilizuia fedha hizo ili mkandarasi afanye kazi kwa viwango stahiki.
"TAKUKURU huokoa fedha kwa kudhibiti ambazo ni taslimu zikiwa zimehamishwa kwenda Upande usio sahihi na kurejesha upande sahihi pia tunaokoa kwa kudhibiti tunaona kuna viashiria vya fedha kiasi fulani zinazotumika kinyume na utaratibu," amesema Celestine.
Mbali na mradi huo pia katika kuhakikisha ubora wa fedha za miradi mwaka 2025 TAKUKURU imeweza kuokoa millioni 195 za CSR kulikuwa na malalamiko ya wamiliki wa leseni za madini walikuwa ucheleweshaji kutoa fedha walizokubaliana na halmashauri ya Musoma Vijijini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya CSR.
TAKUKURU imeweza kuifanyia kazi taarifa aliyotoa Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi mara baada ya kutilia shaka kuwa makusanyo yanayokusanywa hayaendani na hali halisi ya makusanyo yaliyopo pale Mwigobero ndipo waliposhauri uwepo wa mizani pale na mizigo ilipiwe mpaka sasa mapato yameongezeka haya yote ni matokeo ya uchambuzi wa mifumo yanayofanywa na TAKUKURU na kuokoa mapato yanayopotea.
Akimalizia Afisa habari na Mawasiliano wa TAKUKURU mkoa wa Mara Agnes Karatibu amesema ni vema wananchi wakawa na utaratibu wa kufuatilia taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari kwenye vipindi vinavyorushwa ilinkupata elimu sahihi inayohusu masuala ya rushwa na kuweza kutoa taarifa zenye viashiria vya rushwa.
Tukumbushane kauli mbiu ya TAKUKURU inasema "Kuzuia Rushwa ni Jukumu lako na langu,tutimize wajibu wetu".





Comments
Post a Comment