MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amempongeza Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, kwa dhamira yake ya kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, akisema juhudi hizo ni muhimu katika kulinda familia dhidi ya mzigo wa gharama za matibabu.
Kanali Mtambi amesema hatua ya Mbunge huyo kuandaa Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote ni mfano wa uongozi unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, kwa kuwa afya ni msingi wa ustawi wa familia na maendeleo ya jamii.
Akizungumza katika kongamano hilo, Kanali Mtambi amesema bado kuna wananchi ambao hawajaelewa kikamilifu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, hivyo juhudi za viongozi kupeleka elimu kwa wananchi zinapaswa kuungwa mkono.
Amesema Bima ya Afya kwa Wote inatoa kinga dhidi ya changamoto ya gharama kubwa za matibabu ambazo zimekuwa zikizikabili familia nyingi, huku akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kuhakikisha wanapata huduma za afya bila mzigo mkubwa wa gharama.
“Hongera sana Mheshimiwa Mbunge Ghati kwa kufanya jambo muhimu, jambo zuri sana katika jamii, si kwa Watanzania wa Tarime tu, lakini kwa jamii ya Wana Mara wote kwa ujumla,” amesema Kanali Mtambi.
Amesema dhamira ya Ghati Chomete haipaswi kuishia katika kongamano hilo pekee, bali inapaswa kuwa sehemu ya mwendelezo wa kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika Bima ya Afya kwa Wote.
Kanali Mtambi ameeleza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakikosa fursa za kunufaika na mfumo wa bima kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu namna unavyofanya kazi, akisema mikutano na makongamano kama hilo ni muhimu katika kuondoa changamoto hiyo.
Amesema Serikali, viongozi, wadau na wananchi wanapaswa kushirikiana katika kuhakikisha lengo la Bima ya Afya kwa Wote linafikiwa na wananchi wengi zaidi wanapata huduma za afya kwa usawa.
Kanali Mtambi amesisitiza kuwa dhamira ya Ghati Chomete ya kuhamasisha wananchi kuhusu bima ya afya ni jambo linalostahili kuungwa mkono, kwa kuwa linagusa moja kwa moja ustawi wa familia na jamii nzima ya Mara.





Comments
Post a Comment