MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Mhe. Ghati Chomete, ameunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kupitia utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa Mkoa wa Mara umeendelea kutekeleza kwa vitendo zoezi hilo kwa kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya afya.
Akizungumza katika hafla ya Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote lililofanyika mkoani Mara, Mhe. Chomete amesema hatua hiyo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na uhakika wa kupata huduma za afya bila kikwazo cha gharama.
Amesema viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mara wana wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kuwa na bima ya afya na kutumia fursa hiyo kujiunga na mfumo huo.
Mhe. Chomete amempongeza Rais Samia kwa kuweka msukumo mkubwa katika kuboresha sekta ya afya na kusimamia malengo ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na bima ya afya.
“Ninakupongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujikita katika kusimamia malengo makubwa ya kuhakikisha Tanzania na Watanzania wanakuwa na afya njema,” amesema.
Hata hivyo, amesema pamoja na juhudi za Serikali na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote katika Mkoa wa Mara, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu vifurushi vya bima ya afya na huduma wanazostahili kupata.
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikumbana na changamoto wanapofika katika hospitali, ambapo wakati mwingine huambiwa huduma wanayoihitaji haipo katika kifurushi cha bima walichonacho.
Mhe. Chomete, amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa viongozi na wadau wa afya kuendelea kutoa elimu ya kutosha ili mwananchi anayejiunga na bima awe na uelewa wa huduma zinazopatikana katika kifurushi chake.
Amesema wananchi wanapaswa kuelekezwa kwa uwazi kuhusu kifurushi wanachonunua, huduma kinazohusisha na namna ya kunufaika nacho, ili waweze kufanya maamuzi sahihi wakati wa kujiandikisha.
“Tunatakiwa kushusha elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa kifurushi watakachokichukua kina huduma gani, ili mwananchi aweze kuamua kwa uelewa kujiunga au kwenda kujiandikisha kuchukua bima ya afya,” amesema.
Amesema viongozi, hususan wabunge na viongozi wengine katika jamii, wana nafasi kubwa ya kusaidia Serikali katika kutoa elimu hiyo na kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote.
Mhe. Chomete amesisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano wa Serikali, viongozi, wataalamu wa afya na wananchi katika kuhakikisha mfumo wa bima unakuwa na uelewa mpana na unawafikia Watanzania wengi zaidi.





Comments
Post a Comment