MWENYEKITI wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, amesema maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya Bonanza la Bunge–NMB litakalofanyika kesho, Agosti 29, 2026, katika Viwanja vya John Meling, jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Sanga amesema bonanza hilo litaanza saa 12:00 asubuhi, likiwa na ushiriki wa taasisi na wizara mbalimbali za Serikali, huku washiriki wakitarajiwa kuwa wengi zaidi ikilinganishwa na mabonanza yaliyopita.
Amesema bonanza hilo ni sehemu ya jitihada za Bunge kuendeleza michezo miongoni mwa watumishi, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wake.
“Mheshimiwa Spika ametoa msisitizo kwamba Bunge lazima lijishirikishe katika shughuli za michezo, kwa sababu michezo ni muhimu katika kuimarisha afya na kujenga ushirikiano,” amesema Sanga.
Takribani wizara 14 pamoja na taasisi nyingine zaidi ya 10 zimealikwa kushiriki bonanza hilo, hivyo kufanya idadi ya taasisi zinazotarajiwa kushiriki kufikia takribani 24.
Amesema tofauti kubwa ya bonanza hilo ni kwamba limepanua wigo wa ushirikiano kati ya Bunge, taasisi za Serikali na sekta ya kibenki, hususan Benki ya NMB, ambayo imekuwa mshirika muhimu wa Bunge katika shughuli mbalimbali.
Sanga ameiishukuru NMB kwa udhamini na ushirikiano wake katika kufanikisha bonanza hilo, akisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Bunge katika kuandaa shughuli za michezo kwa takribani miaka minne mfululizo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika michezo na kufanya mazoezi, akieleza kuwa mtindo bora wa maisha na mazoezi husaidia kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Katika bonanza hilo, michezo mbalimbali inatarajiwa kufanyika, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa kikapu na kuvuta kamba, huku timu za Bunge zikikutana na taasisi na wizara mbalimbali.
Miongoni mwa taasisi na wizara zitakazoshiriki ni NMB, Wizara ya Afya, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Nishati, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Maji, Mahakama, UDOM, TRA, WCF, DUWASA, PPRA, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) pamoja na taasisi nyingine.
Sanga amesema Bunge limejiandaa kikamilifu kwa bonanza hilo, ambapo viwanja mbalimbali vimeandaliwa na vifaa muhimu, ikiwemo kombe na medali, vimepokelewa kutoka NMB.
Ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuunga mkono bonanza hilo, akisema litakuwa fursa muhimu ya kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Serikali na taasisi mbalimbali.
Kwa upande wake Mshauri Mwandamizi wa Kitengo cha Biashara za Serikali, NMB Bank Bi. Vicky Bishubo, amesema michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga afya, upendo na mshikamano katika jamii, huku ikichangia kuongeza tija katika maeneo ya kazi.
"NMB Bank inaamini katika kurejesha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii kupitia shughuli mbalimbali zenye manufaa, ikiwemo michezo". amesema
Amesema michezo inapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa pamoja na kuboresha afya za watu, inajenga mahusiano mema, mshikamano na ushirikiano, mambo ambayo yana mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na tija katika maeneo ya kazi.
“Michezo ni afya, michezo inakuza upendo, michezo inaongeza mshikamano, michezo pia inaongeza tija, kwa sababu wanaoshiriki katika michezo wakiwa na afya njema, basi na tija katika maeneo ya kazi inaongezeka,” amesema Bishubo.
Bunge Bonanza linatarajiwa kufanyika kesho, Agosti 29, 2026, katika Viwanja vya John Melin jijini Dodoma, likihusisha michezo mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za michezo na mazoezi huku Mgeni rasmi katika bonanza hilo anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Zungu.



Comments
Post a Comment