Abiria wanaosafiri kati ya Mikoa ya Mwanza, Geita, Kigoma na Kagera wamelipongeza Jeshi la Polisi Mikoa ya Mwanza na Geita kwa operesheni kabambe ya kushtukiza iliyolenga mabasi ya abiria na magari mengine ya usafirishaji, wakisema hatua hiyo inalinda maisha yao na kurejesha nidhamu barabarani.
Pongezi hizo zimetolewa kufuatia operesheni ya pamoja iliyofanyika Oktoba 9 na kuongozwa na Wakuu wa Vikosi vya Usalama Barabarani wa mikoa hiyo miwili, ambapo zaidi ya magari 100 yalikaguliwa, ikiwa ni pamoja na mabasi 38 ya abiria.
Wakizungumza wakati wa operesheni hiyo, baadhi ya abiria walieleza kuwa hatua hizo za kushtukiza zinapaswa kufanyika mara kwa mara ili kudhibiti ajali za barabarani ambazo zinaweza kuzuiliwa kwa kuongeza usimamizi.
"Tunamshukuru sana Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani na askari wake. Dereva anapojua kuna ukaguzi wa kushtukiza anakuwa makini sana. Hatua hii inalinda roho zetu kwa sababu ajali nyingi zimekuwa zikitokea kwa uzembe wa madereva wanaolewa na kujaza abiria kupita kiasi," alisema Boniphace Mathias abiria aliyekuwa kwenye basi akitokea Mwanza kwenda Katoro.
Katika ukaguzi huo, wakuu hao wa usalama barabarani walibaini changamoto kadhaa zinazohatarisha usalama wa abiria, ikiwemo baadhi ya madereva kuendesha wakiwa wamezidisha abiria kuliko uwezo wa gari, ukiukwaji wa sheria za barabarani, pamoja na mabasi ya masafa marefu kutokuwa na madereva wawili.
Kufuatia kubainika kwa makosa hayo, mbali na kuchukua hatua za kisheria, pia walitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa madereva kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani na kuzingatia takwa la kuwa na madereva wawili kwa safari ndefu ili kuepuka uchovu unaosababisha ajali.
Akizungumzia operesheni hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mathayo Msuyale, alisema kuwa zoezi hilo si la siku moja bali ni endelevu ili kuhakikisha usalama unadumishwa muda wote.
"Hii ni operesheni ya kawaida na ni endelevu. Hatutavumilia dereva yeyote anayechezea maisha ya wananchi. Tutahakikisha kila gari linaloingia na kutoka katika mikoa ya kanda hii linakuwa salama na linasafiri kulingana na sheria," amesisitiza ACP Msuyale.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sunday Ibrahim, aliongeza kuwa operesheni hiyo inalenga moja kwa moja kutokomeza tabia za hatari kama vile ulevi na uendeshaji wa hatari, huku akibainisha kuwa wataendelea kushirikiana kwa karibu na mikoa jirani ili kubana mianya yote ya ukiukwaji wa sheria za barabarani na kupunguza ajali.






Comments
Post a Comment