MKUU wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi, amelitaka Jeshi la Akiba Mkoa wa Mara kuandaa na kutunza taarifa za watu wote waliowahi kupata mafunzo ya mgambo, hatua itakayosaidia kuwa na kanzidata ya watu wenye ujuzi wa msingi wa ulinzi na usalama kwa ajili ya matumizi mbalimbali pale inapohitajika.
Brigedia Jenerali Mtambi ametoa agizo hilo leo Oktoba 5, 2026, alipompokea Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Mara, Kanali Zacharia Godfrey Kitani, aliyefika kujitambulisha baada ya kuhamia katika Mkoa wa Mara.
Katika mapokezi hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amelipongeza Jeshi la Akiba kwa kazi linayoifanya katika kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, akieleza kuwa lina nafasi muhimu katika kuhakikisha amani, utulivu na usalama wa wananchi vinaendelea kulindwa.
Amesema Jeshi la Akiba ni sehemu muhimu ya mfumo wa ulinzi wa nchi, hivyo linapaswa kuendelea kujiimarisha na kuwa na mipango madhubuti itakayowezesha kutumia vizuri watu waliopata mafunzo ya mgambo katika maeneo mbalimbali.
“Jeshi la Akiba linapaswa kujipanga vizuri, kuandaa na kutunza taarifa za watu wote waliowahi kupata mafunzo ya mgambo,” amesema Brigedia Jenerali Mtambi, huku akisisitiza umuhimu wa taarifa hizo katika kurahisisha utambuzi na upatikanaji wa watu wenye mafunzo pale wanapohitajika.
Aidha, amelitaka Jeshi la Akiba kusimamia na kushirikiana na taasisi za ulinzi na usalama katika kuhakikisha watumishi wenye mafunzo ya mgambo wanapewa fursa za kuajiriwa, ili kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi na uzoefu katika taasisi hizo.
Brigedia Jenerali Mtambi amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kutumia ipasavyo rasilimali watu waliopo ndani ya Mkoa wa Mara, sambamba na kuendelea kujenga uwezo wa wananchi katika kushiriki katika masuala ya ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mtambi amesema Mkoa wa Mara umeanza kufufua kamati mbalimbali za kisheria katika ngazi za kata, vijiji, mitaa na vitongoji, kwa lengo la kuhakikisha kamati hizo zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Amesema kamati hizo zina nafasi muhimu katika kushughulikia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo ya wananchi, hivyo ni muhimu viongozi na wajumbe wake kutambua majukumu yao na kuyatekeleza kwa ufanisi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa usalama wa wananchi hauwezi kuwa jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali unahitaji ushirikiano wa viongozi katika ngazi zote pamoja na wananchi wenyewe.



Comments
Post a Comment