NAIBU Waziri wa Utumishi na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Mhe. Regina Ndege, amewafikia kinamama waliojifungua katika Kituo cha Afya Dareda Kati, Wilaya ya Babati Vijijini, kwa kutoa msaada mbalimbali wa kiutu pamoja na mablanketi 30 kwa ajili ya kituo hicho.
Regina ametoa msaada huo Oktoba 3, 2026 alipokuwa Mgeni Rasmi katika Sherehe za Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Babati Vijijini, chini ya Mwenyekiti wa UWT Wilaya hiyo, Ndg. Agata.
Akiwa katika Kituo cha Afya Dareda Kati, Regina ametembelea kinamama waliokuwa wamejifungua na kuwapatia msaada mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuunga mkono katika kipindi hicho muhimu cha maisha yao.
Aidha, alikabidhi mablanketi 30 kwa ajili ya matumizi ya kituo hicho, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Baada ya kutembelea kituo hicho, Regina alifika katika Shule ya Msingi Dareda Kati, ambako alikutana na wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuwapatia mahitaji ya msingi pamoja na zawadi mbalimbali.
Katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya UWT, Regina alishiriki mkutano mkubwa uliohudhuriwa na viongozi na wanachama wa UWT pamoja na wananchi mbalimbali.
Katika mkutano huo, amekabidhi bati 20 kwa ajili ya ujenzi wa banda la kuku katika Shule ya Msingi Dareda Kati, ikiwa ni sehemu ya kusaidia shughuli za uzalishaji na maendeleo ya shule hiyo.
Pia, Regina ametoa Shilingi milioni moja kwa vijiji vinne vilivyowasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa matenti yatakayotumika wakati wa maafa, hatua inayolenga kuimarisha maandalizi ya jamii kukabiliana na changamoto za maafa.
Ziara na misaada hiyo ilikuwa sehemu ya shughuli za Wiki ya UWT Wilaya ya Babati Vijijini, ambazo pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano, zililenga kugusa maisha ya wananchi na kuchochea shughuli za maendeleo katika jamii.

























Comments
Post a Comment