Kuhusu ushiriki, Mnyeti amesema mwaka huu washiriki 765 kutoka sekta binafsi na sekta ya umma wamejitokeza, wakiwemo kampuni za uchimbaji 15, taasisi za umma 41, wajasiriamali 599, wachimbaji wadogo 52, taasisi za fedha 7 na watoa huduma mbalimbali 51.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Pastory Mnyeti ametangaza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini.
Akizungumza Leo Septemba 26,2026 katika Viwanja vya Dkt. Samia Mkoani Geita, Mnyeti alisema maonesho hayo yaliyoanza Septemba 23, 2026 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba 27 na kufungwa Oktoba 03, 2026.amesema maonesho ya mwaka huu yanabeba Kauli Mbiu isemayo "Madini ni Utajiri tuwajibike kwa pamoja kufikia Dira ya Taifa 2050" inayolenga kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia katika uzalishaji wa madini ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
"Lengo kuu ni kuhakikisha ifikapo 2035 tunakuwa na maonesho bora ya teknolojia ya madini na sekta fungamanishi barani Afrika. Tunamkaribisha sana Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Mwinyi kuja kutuunga mkono," alisema Mnyeti.
Amefafanua kuwa malengo mahususi ni kukuza matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji, kuwaunganisha wazalishaji na wasambazaji wa teknolojia na wachimbaji, kuwaunganisha wachimbaji na taasisi za Serikali na wadau wa mazingira, pamoja na kuwakutanisha wawekezaji wakubwa na wadogo kutafuta suluhu ya changamoto zao.
Ameishukuru Serikali na wadau wote waliodhamini maonesho hayo na kuwataka wananchi wa Geita kujitokeza kwa wingi kumpokea mgeni rasmi na kunufaika na fursa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa madini.





Comments
Post a Comment