KUTOKANA na Serikali kuendelea kuwahimiza vijana nchini kujiajiri kupitia taaluma zao, mhitimu mmoja wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Nicolaus Carol Mboya, ameonesha kwa vitendo namna maarifa anayoyapata darasani yanavyoweza kugeuzwa kuwa biashara na hatimaye kuunda ajira kwa vijana wengine.
Mboya, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uhasibu wa Umma na Fedha katika Kampasi ya Dar es Salaam, alianza safari yake ya ujasiriamali akiwa bado mwanafunzi wa mwaka wa tatu mwaka 2025, baada ya kushinda Shindano la Wazo la Biashara lililoendeshwa na TIA.
Ushindi huo ulimpa fursa ya kwenda nchini Uganda kujifunza na kupata uzoefu zaidi kuhusu biashara na ubunifu, jambo lililomsaidia kukuza na kuboresha wazo lake hadi kufikia hatua ya kulifanya kuwa biashara halisi.
Mwaka 2026, wazo hilo lililozaliwa akiwa mwanafunzi liligeuka kuwa kampuni rasmi kupitia kuanzishwa kwa STEAMORA COMPANY LIMITED, kampuni ya teknolojia ya elimu (EdTech) iliyozinduliwa rasmi Aprili 1, 2026.
Kupitia bidhaa yake kuu ya SPARKS 360° HUB, STEAMORA inawawezesha watoto na vijana wenye umri wa miaka 3 hadi 17 kujifunza kwa vitendo katika maeneo mbalimbali ya sayansi na teknolojia, yakiwemo Robotics, Coding and Programming, 3D Design and Printing, Electric Circuits, Science Projects, Creative Arts pamoja na STEAM yenye Artificial Intelligence (AI).
Kampuni hiyo inalenga kuwajengea watoto na vijana ujuzi wa teknolojia, ubunifu, uwezo wa kutatua changamoto, kufikiri kimantiki na kujiamini katika kuunda suluhisho zao wenyewe, badala ya kuwa watumiaji wa teknolojia pekee.
Tangu kuanzishwa kwake, STEAMORA imewafikia zaidi ya wanafunzi 600 kupitia ushirikiano na shule nane za kimataifa pamoja na vituo viwili vya kujifunzia vya kijamii jijini Dar es Salaam.
Aidha, kampuni hiyo kwa sasa ina watumishi wanane na imezalisha zaidi ya Sh milioni 15 katika mapato, jambo linaloonesha namna wazo la mwanafunzi lilivyoweza kukua na kuwa biashara yenye kutoa ajira na kuchangia uchumi ndani ya muda mfupi.
Akielezea mafanikio hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Amos Pallangyo, amesema mfano wa Nicolaus ni miongoni mwa matokeo ambayo taasisi hiyo inalenga kuyafikia katika kuwaandaa wanafunzi kwa soko la ajira na ujasiriamali.
“Hii ni baadhi ya mifano halisi ya kile TIA inacholenga kufikia; mwanafunzi kuingia darasani akiwa na maarifa na kutoka akiwa na uwezo wa kutengeneza suluhisho, kuanzisha biashara na kuunda ajira,” amesema Prof. Pallangyo.
Prof. Pallangyo amesema TIA imeendelea kuongeza fursa kwa wanafunzi na watumishi kushiriki katika programu na shughuli mbalimbali za kimataifa, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kwa uchumi unaozidi kuunganishwa duniani.
Amesema wanafunzi wanane (8) wameshiriki programu za Semester Exchange nchini Lithuania, huku wanafunzi 13 wakishiriki katika makongamano ya kimataifa na wengine 74 kushiriki ziara za kitaaluma nchini Kenya, Uganda na Afrika Kusini.
Aidha, watumishi watano (5) wa kitaaluma wameshiriki programu za kimataifa za kubadilishana ufundishaji.
Kwa upande mwingine, TIA imeendelea kutoa madarasa ya lugha za Kichina na Kirusi katika Kampasi ya Dar es Salaam, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa mawasiliano na kuongeza fursa zao katika mazingira ya kimataifa ya biashara na ajira.
Katika eneo la teknolojia, TIA imeendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA kupitia Student Information Management System (SIMS), mfumo uliochukua nafasi ya mfumo wa zamani wa SMS.
Prof. Pallangyo amesema mfumo huo unasimamia huduma za wanafunzi kuanzia maombi ya kujiunga, udahili na usajili, hadi malipo, matokeo, transcript na taarifa mbalimbali za kitaaluma.




Comments
Post a Comment