KAMISHNA Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika Idara ya Uhamiaji, akisema hatua hizo zimeongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wageni wanaoingia na wanaotoka nchini.
Dkt. Makakala amesema maboresho hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, hususan katika kusimamia shughuli za uhamiaji, udhibiti wa wageni pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi na wageni wanaofika nchini.
Dkt. Makakala Ameyasema hayo wakati akizungumza katika Kikao Kazi cha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na Maafisa Uhamiaji wa Mikoa, kilichofanyika mkoani Kilimanjaro, kikao kilicholenga kutathmini utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026, pamoja na kupitia utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Dkt. Makakala, amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho yametokana kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji unaotolewa na Serikali, hususan katika eneo la bajeti na uwekezaji katika teknolojia za kisasa zinazolenga kurahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma za uhamiaji.
*matumizi ya teknolojia yameendelea kubadilisha namna huduma zinavyotolewa katika Idara hiyo, kwa kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kuhudumia wasafiri na kuwezesha mifumo ya uhamiaji kufanya kazi kwa ufanisi zaidi". Amesema
“Maboresho haya yaliyochagizwa na uwezeshaji wa kibajeti pamoja na matumizi ya teknolojia yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye mifumo mizuri ya utoaji huduma katika eneo la uhamiaji,” ameongeza Dkt. Makakala.
Amesema hatua hizo pia zimeongeza uwezo wa Idara ya Uhamiaji katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika shughuli za uhamiaji, huku ikihakikisha kuwa wageni wanaoingia na kutoka nchini wanapata huduma kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi.
Aidha, Dkt. Makakala amewataka Maafisa Uhamiaji katika mikoa kuendelea kusimamia kwa weledi majukumu yao na kuhakikisha maboresho yaliyofanyika yanaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi, wageni na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi wa Idara hiyo kuendelea kutumia teknolojia na mifumo iliyoboreshwa katika kutoa huduma, huku wakizingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kikao hicho cha Kazi pia kimetoa nafasi ya kupitia mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha zaidi utendaji wa Idara ya Uhamiaji katika mwaka wa fedha 2026/2027, sambamba na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na huduma bora na mifumo ya kisasa ya uhamiaji barani Afrika.





Comments
Post a Comment