Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuelekeza uwekezaji wake katika maeneo ya kimkakati yatakayochochea mageuzi ya sekta ya kilimo na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza Agosti 2, 2026, baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Balozi Khamis alisema maendeleo ya sekta ya kilimo ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.
Amesema Serikali imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuimarisha sekta hiyo kwa kuongeza mtaji wa TADB kutoka shilingi bilioni 60 hadi zaidi ya shilingi bilioni 400, hatua itakayoiwezesha benki hiyo kuongeza uwezo wa kufadhili miradi ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu kwa kiwango kikubwa zaidi.
"Mafanikio ya sekta ya kilimo yatachangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Hivyo, TADB inapaswa kuelekeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati yatakayoongeza tija, thamani ya mazao na manufaa kwa wananchi pamoja na uchumi wa taifa," amesema Balozi Khamis.
Ameeleza kuwa Serikali inalenga kutumia sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu kama nguzo muhimu za kukuza uchumi, kupunguza umaskini, kuongeza ajira na kipato cha wananchi, pamoja na kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa dola trilioni moja kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo kuongeza juhudi za kuwatafutia wakulima na wazalishaji masoko ya uhakika ya bidhaa zao, sambamba na kuwawezesha kuongeza uzalishaji wenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.
Balozi Khamis pia ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuendeleza sekta hiyo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwa nguvu katika kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza tija, kuimarisha usalama wa chakula, kuzalisha ajira nyingi zaidi na kuinua kipato cha wananchi.
Ziara ya Waziri huyo katika banda la TADB imeonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha taasisi za kifedha zinazowezesha maendeleo ya sekta ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya sekta hiyo kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Comments
Post a Comment