Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwa na misingi mizuri ya kiuchumi, hali inayoweka mazingira bora ya kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 03, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na kushiriki katika mkutano wa mazungumzo maalum na sekta binafsi kuhusu utekelezaji wa dira hiyo.
Amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa himilivu, mfumuko wa bei umedhibitiwa, uwekezaji umeongezeka na nchi imeendelea kujenga nafasi yake kama lango muhimu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Ukanda wa Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.
“Ni muhimu kutambua tumeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 tukiwa na msingi mzuri wa kiuchumi. Uchumi wetu umeendelea kuwa himilivu, mfumko wa bei unadhibitiwa, uwekezaji umeongezeka na Tanzania imeendelea kujenga nafasi yake kama lango la biashara,” amesema Rais Samia.
Amesema msingi huo unatoa fursa kwa Tanzania kusonga mbele katika safari ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na himilivu unaowanufaisha wananchi wote.
Rais Samia amesisitiza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 utahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi, ambayo imepewa nafasi kubwa katika kuchochea uwekezaji, uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kitaasisi ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya maendeleo.












Comments
Post a Comment