Na MASHAKA MHANDO, Tanga
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kali kwa wamiliki wa blogu, tovuti (websites), na mawakala wa habari mtandaoni wanaosambaza habari bila kusajiliwa na kupata leseni, ikieleza kuwa wanafanya makosa ya jinai na watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hata hivyo, ili kuweka mazingira rafiki, TCRA imetangaza kushusha gharama za usajili na kupata leseni kutoka Shilingi 500,000 za awali hadi Shilingi 50,000 pekee, ili kutoa fursa kwa kila mwandishi wa mtandaoni kutambulika kisheria.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TCRA, Rolf Kibaja, wakati akizungumza kwenye Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika jijini Tanga.
Kibaja aliwataka wamiliki hao kutojidanganya kuwa hawajulikani, akisisitiza kuwa TCRA ina mfumo thabiti wa kufuatilia anga mtandao (Cyberspace) ambao kila baada ya saa sita hutoa taarifa za kile kinachorushwa, ambapo hadi sasa wanaona utendaji wa runinga za mtandaoni (Online TV) zipatazo 400 pamoja na blogu zote zisizosajiliwa.
Tofauti ya sheria: Aliyesajiliwa na Asiyesajiliwa
Akifafanua kuhusu umuhimu wa leseni hiyo, Kibaja alisema kuwa inampa mwandishi ulinzi tofauti na yule anayefanya kazi kinyemela ambapo mwenye Leseni akifanya kosa la kimaudhui, ataitwa na Kamati ya TCRA na kuonywa au kupewa adhabu ya kikanuni.
Tofauti na asiye na leseni Kibaja alisema yeye havunji kanuni bali anavunja sheria za nchi, hivyo hatashughulikiwa na TCRA, bali atakamatwa na Jeshi la Polisi na kukabiliwa na makosa ya kimtandao (Cybercrimes).
Watengeneza Maudhui (Content Creators) Wasamehewa
Pamoja na msimamo huo mkali, TCRA imeweka wazi kuwa Watengeneza Maudhui Mtandaoni (Content Creators)—kama vile wachekeshaji na waigizaji—hawalipi na hawapaswi kuwa na leseni, kwa sababu kazi wanazozifanya zinahesabika kama ubunifu binafsi na siyo usambazaji wa habari rasmi.
Maelekezo kwa Wabunifu wa Mashine
Katika hatua nyingine, Bw. Kibaja amewataka wataalamu na vijana wanaobuni mashine mbalimbali zinazohitaji kuwasiliana na mashine nyingine (Internet of Things), kufika TCRA ili kupewa namba za mawasiliano bure, jambo ambalo ni takwa la kisheria na kiusalama.
Mkakati wa Vijana na 'Girls in ICT'
Kuelekea Dira ya Taifa ya miaka 25 ijayo, TCRA imeanza mkakati kabambe wa kuandaa vijana kiteknolojia ili waendane na matumizi ya Akili Mnemba (AI) na kubuni programu tumishi (Apps) zinazotatua changamoto za Kitanzania kama vile kilimo, udongo, na mimea.
"Kwa mujibu wa Sensa ya 2022, asilimia 70 ya Watanzania ni vijana. Tukiwapika vizuri kwenye masuala ya kidijitali na usalama wa kimtandao, wataleta manufaa makubwa sana. Hii ndiyo maana tumeanzisha klabu 780 kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu kuhamasisha matumizi ya kidijitali," alisema Kibaja.
Alimalizia kwa kugusia programu maalum ya 'Girls in ICT' inayoendeshwa na mamlaka hiyo, ikilenga kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi na TEHAMA ili kuondoa utawala wa wanaume pekee katika sekta hiyo, akisisitiza kuwa wanawake wana uwezo mkubwa endapo wataandaliwa vizuri kisaikolojia na kielimu.



Comments
Post a Comment