Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya. amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1975 kama kitengo cha Shirika la Usafirishaji la Taifa, kabla ya kupandishwa hadhi mwaka 1982 kuwa taasisi ya elimu ya juu yenye jukumu la kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika sekta ya uchukuzi.
Amesema baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Tanzania ilikabiliwa na uhaba wa wataalamu wa sekta ya usafirishaji, hali iliyoifanya Serikali kuimarisha chuo hicho ili kiweze kuzalisha wataalamu wa usafiri wa barabara, reli, anga na majini.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika sekta ya uchukuzi, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ujenzi na ukarabati wa meli pamoja na kuboresha viwanja vya ndege.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Chuo, miradi hiyo imeongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi, hivyo NIT imepanua programu zake za masomo ili kuzalisha wahitimu watakaosimamia na kuendesha miundombinu hiyo kwa ufanisi.
Amesisitiza kuwa sekta ya uchukuzi ndiyo mhimili wa maendeleo ya uchumi wa taifa, na kwamba uwekezaji katika elimu ya wataalamu wa sekta hiyo ni msingi muhimu wa kuhakikisha miradi mikubwa ya Serikali inaleta tija kwa Watanzania.









Comments
Post a Comment