Na Mashaka Mhando, MWANZA
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imeahidi kumaliza changamoto ya ukosefu wa taa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ili kuwezesha uwanja huo mkongwe kutumika kwa mechi na matamasha nyakati za usiku.
Ahadi hiyo nzito imetolewa leo, Agosti 8, 2026, na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma (maarufu Mwana FA), wakati alipofanya ziara maalum ya kukagua miundombinu ya uwanja huo, huku akisisitiza kushirikiana na wadau wa michezo kutatua kero hiyo.
Mhe. Mwinjuma amebainisha kuwa dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha miundombinu yote ya michezo nchini inaboreshwa na kufikia viwango vinavyokidhi mahitaji ya sasa.
"Moja ya changamoto kubwa iliyopo hapa Kirumba ni ukosefu wa mfumo wa taa unaowezesha uwanja kutumika kwa ufanisi nyakati za usiku. Hali hii imekuwa ikipunguza fursa za kufanyika kwa baadhi ya shughuli za michezo, hususan mechi na matukio yanayohitaji matumizi ya uwanja wakati wa usiku, naahidi hili nitalifanyia kazi," alisema Mhe. Mwinjuma.
Ziara na Viongozi wa Chama
Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Naibu Waziri aliambatana na Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, ikiongozwa na Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Bw. Abdul Mtua.
Viongozi hao walipata fursa ya kujionea hali halisi ya uwanja huo na kujadili kwa kina mikakati ya kushughulikia changamoto zilizopo, lengo likiwa ni kuongeza thamani ya uwanja huo kwa manufaa ya wananchi na wadau wa michezo Kanda ya Ziwa.
Hatua ya uboreshaji wa Uwanja wa CCM Kirumba inaenda sambamba na msisitizo na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayoendelea kuwekeza nguvu kubwa katika kuboresha miundombinu ya michezo nchini ili iwe salama na itumike ipasavyo kuzalisha ajira na vipaji vipya.








Comments
Post a Comment