Na Prosper Makene
Dar es Salaam, Tanzania – Jumamosi, 1 Agosti 2026: Serikali imeipongeza Stanbic Bank Tanzania kwa mchango wake wa muda mrefu katika kuunga mkono michezo nchini, hususan kupitia udhamini wa Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga. Mashindano hayo yamedhaminiwa na Stanbic Bank kwa Shilingi milioni 30.
Msigwa alisema ushiriki wa sekta binafsi katika michezo ni muhimu kwa kuwa unasaidia kukuza vipaji, kuimarisha afya ya jamii na kujenga mahusiano baina ya watu.
"Naipongeza Stanbic Bank kwa kuendelea kudhamini mashindano haya kwa miaka mingi. Ushirikiano wa namna hii kati ya sekta binafsi na jamii unachangia kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa mataifa yetu mawili na kudhihirisha urafiki wa kudumu uliopo kati ya China na Tanzania," alisema Msigwa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, ambaye alishuhudia ukabidhi wa hundi ya udhamini kutoka Stanbic Bank.
Mbali na kuwa mdhamini mkuu, Stanbic Bank pia imetoa timu yake kushiriki mashindanoni. Ushiriki huo umeonyesha dhamira ya benki ya kuwa karibu na jamii na kushiriki moja kwa moja katika shughuli zinazowaunganisha watu.
Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Corporate and Investment Banking) wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema udhamini huo unaakisi imani ya benki katika nguvu ya michezo kama chombo cha kuunganisha watu.
"Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa muhimu kwetu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee. Dhamira hiyo ndiyo msingi wa kazi yetu kupitia Standard Bank Group, ushirikiano wetu na ICBC pamoja na dawati letu maalum la huduma kwa wafanyabiashara wa Kichina," alisema Manase.
Aliongeza kuwa:
"Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Tunaendelea kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja."
Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Wachina yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya biashara, kuimarisha mahusiano na kukuza kubadilishana uzoefu wa kitamaduni kati ya wadau kutoka Tanzania na China.
Kadri ushirikiano huo unavyoendelea kukua, Stanbic Bank itaendelea kuimarisha uhusiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania pamoja na kuunga mkono majukwaa yanayochochea ushirikiano, maelewano na maendeleo ya pamoja.

Comments
Post a Comment