MBUNGE wa Jimbo la Serengeti, Mheshimiwa Mary Daniel Surati, amekabidhi gari kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Serengeti ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utendaji wa shirika hilo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme kwa wananchi.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika Julai 31, 2026, yanatarajiwa kusaidia TANESCO kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi katika utekelezaji wa miradi ya umeme pamoja na kuboresha huduma kwa wakazi wa Serengeti.
Baada ya hafla hiyo, Mbunge Surati alikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umeme cha Nyamongo Mugumu (Nyamongo Mugumu Power Station), mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 3.9 unaotekelezwa kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika wilayani humo.
Akiwa eneo la mradi, ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma bora ya umeme. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 30, 2026.
Mheshimiwa Surati amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, uwekezaji, viwanda vidogo, biashara pamoja na kuboresha huduma za kijamii kama elimu na afya katika Wilaya ya Serengeti.
Kwa niaba ya wananchi wa Serengeti, Mbunge huyo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya nishati na kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha huduma muhimu za maendeleo zinawafikia wananchi wote, huku miradi ya umeme ikiwa miongoni mwa vipaumbele vinavyochochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.







Comments
Post a Comment