MBUNGE wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Mary Daniel Surati, amekabidhi shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti, zinazojengwa Mugumu.
Mhe. Surati amekabidhi fedha hizo leo, Alhamisi, Agosti 13, 2026, akieleza kuwa ujenzi wa ofisi bora utasaidia kuimarisha utendaji, uratibu na shughuli mbalimbali za Chama katika Wilaya ya Serengeti.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na viongozi, wanachama pamoja na wadau mbalimbali katika kusukuma mbele juhudi za maendeleo ya Serengeti.
Katika makabidhiano hayo, imeelezwa kuwa Maendeleo Magereza Mugumu watasimamia na kutekeleza ujenzi wa mradi huo hadi kukamilika.
Mhe. Surati ametoa wito kwa viongozi, wanachama na wadau wa CCM kuendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi zinazolenga kuhakikisha ujenzi wa ofisi hizo unakamilika kwa wakati.
“Ninaendelea kusimamia kwa vitendo dhamira yangu ya kushirikiana na wananchi na taasisi mbalimbali katika kuleta maendeleo ya Serengeti,” amesema Mhe. Surati.
Ameongeza kuwa uwepo wa ofisi hiyo utakuwa sehemu muhimu katika kuimarisha mazingira ya utendaji na utekelezaji wa shughuli za Chama katika Wilaya hiyo.
Kauli mbiu ya Jimbo la Serengeti INASEMA kuwa Serengeti Yetu, Maendeleo Yetu.




Comments
Post a Comment