Katibu Mkuu @maendeleoyajamii, Eliakimu Maswi na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi M. Kida, leo Agosti 20, 2026 wamejadiliana kuhusu ufungamanishaji wa Ajenda ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kijamii na Maendeleo ya Mtaji Watu katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Dira 2050.
Majadiliano yao yamejikita katika umuhimu wa kuhakikisha mipango na mikakati ya kisekta hususani sekta ya maendeleo ya Jamii, inaendana na vipaumbele vya Taifa vilivyowekwa katika Dira 2050 na mipango ya maendeleo ya muda mrefu na muda wa kati, ili iweze kutoa mchango unaopimika katika kufikia malengo ya Taifa.
Dkt. Kida amesema baada ya Dira 2050 kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, na kuzinduliwa kwa nyenzo za utekelezaji wake Agosti 3, 2026, ni muhimu kila taasisi na mdau kuhakikisha mikakati na programu zake zinafungamana na malengo ya Dira hiyo.
“Nikupongeze Katibu Mkuu Maswi kwa kuchukua hatua ya kuoanisha mikakati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Dira 2050 pamoja na mipango ya Taifa. Hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha masuala ya maendeleo ya jamii yanakuwa sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya Taifa,” amesema Dkt. Kida.
Kwa upande wake, Bw. Maswi amesema Wizara ilianza maandalizi ya utekelezaji wa Dira 2050 Juni 11, 2026, kwa kuunda timu maalum iliyofanya uchambuzi wa Dira hiyo na kuandaa mwelekeo wa Wizara katika kuitekeleza.
Amesema Jamii Ajenda 2050, ni nyenzo ya Wizara hiyo itakayolenga kuchochea utekelezaji wa Dira 2050 kwa upande wa sekta anazosimamia.



Comments
Post a Comment