Kamishna wa Polisi Jamii, CP Alex Mkama, leo Agosti 4, 2026, ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa.
Akimkaribisha, Mkalipa amesema Mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa salama na wenye utulivu, hali inayowawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila hofu. Amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano imara kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
Aidha, amemhakikishia CP Mkama kuwa Mkoa wa Mwanza uko tayari kuendelea kupokea ushauri, maelekezo na miongozo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ili kuimarisha utekelezaji wa falsafa ya Polisi Jamii na kudumisha amani na usalama.
Kwa upande wake, CP Mkama amesema ziara yake inalenga kutathmini utekelezaji wa shughuli za Polisi Jamii mkoani Mwanza, kupitia mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya usalama.
Amesema pia amekuja kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Polisi Jamii zinazofanyika mkoani humo kwa lengo la kuziimarisha na kuongeza ufanisi wake.
CP Mkama amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano na miongozo anayoendelea kutoa kwa Jeshi la Polisi, akieleza kuwa imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa jeshi hilo na kudumisha usalama wa wananchi.
Vilevile, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani Mwanza, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ndio msingi wa mafanikio ya falsafa ya Polisi Jamii.
"Ushirikiano unaooneshwa na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi ndiyo tafsiri halisi ya Polisi Jamii, kwa kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja," amesema CP Mkama.











Comments
Post a Comment