Geita
Benki ya Azania imekutana na wateja na wadau wake kutoka Geita, Katoro na Nyarugusu katika hafla maalum iliyolenga kuimarisha mahusiano, kusikiliza mahitaji ya wateja na kujenga ushirikiano zaidi katika kukuza biashara na shughuli za kiuchumi mkoani Geita.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya, Ndg. Yahaya Mbanka-Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, aliwashukuru wateja kwa imani yao kwa Benki na kusisitiza dhamira ya Azania Bank kuendelea kuwa mshirika wa ukuaji wa biashara zao kupitia huduma mbalimbali ikiwemo akaunti za biashara, mikopo ya mtaji na ufadhili wa ununuzi wa vifaa na mali.
Mgeni Rasmi, Mhe. Martine Shigela, Mkuu wa Mkoa Mteule wa Manyara ambaye hadi uteuzi wake wa hivi karibuni amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, alitoa rai kwa wananchi na wafanyabiashara wa Geita kuendelea kushirikiana na Benki ya Azania na kutumia huduma zake za kifedha kama nyenzo ya kukuza na kuendeleza biashara zao.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Mhe. Leornard Bugomola, alipongeza jitihada za Benki za kuwa karibu na wateja na kuwapatia elimu ya kifedha kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali, zikiwemo akaunti, mikopo, bima pamoja na suluhisho zinazowawezesha kukuza biashara zao.
*Azania Bank – Benki Inayozidi Matarajio.*










Comments
Post a Comment