Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha ubora wa uongozi kwenye sekta ya elimu nchini kwa kuwajengea uwezo viongozi na watendaji kupitia mafunzo ya kitaalamu, tafiti na ushauri elekezi unaolenga kuongeza ufanisi wa usimamizi wa taasisi za elimu.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27 katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, amesema taasisi hiyo imeendelea kutoa programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha viongozi wa elimu kukabiliana na changamoto mpya za sekta hiyo, ikiwemo matumizi ya teknolojia, usimamizi wa rasilimali, utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa na uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Amesema kwa zaidi ya miaka 25 ya utekelezaji wa majukumu yake, ADEM imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuandaa viongozi wenye uwezo wa kusimamia mabadiliko na kusaidia Serikali kufikia malengo ya kujenga mfumo bora wa elimu nchini.
“Uongozi bora wa elimu ni msingi wa kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wataalamu wenye maarifa, ujuzi na ubunifu unaohitajika katika maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Maulid.
Ameeleza kuwa ADEM, ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kuwafikia viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya shule hadi mikoa.
Kwa mujibu wa Dkt. Maulid, kuanzia mwaka 2002 hadi 2025, jumla ya viongozi 8,599 wamehitimu programu ya Stashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu (DELMA), huku viongozi 2,263 wakihitimu programu ya Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) kati ya mwaka 2016 na 2025.
Aidha, kupitia Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST), ADEM imeendesha mafunzo kwa walimu wakuu 17,817, waratibu elimu kata zaidi ya 3,900, pamoja na maafisa elimu wa mikoa na wilaya.
Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano na VVOB Education for Development, ADEM imeanza kutekeleza programu ya miaka mitano (2026–2031) itakayolenga kuwajengea uwezo viongozi wa shule za sekondari nchini, ambapo inatarajiwa kuwafikia wakuu wa shule zaidi ya 12,000 pamoja na wasimamizi wengine wa elimu.
Dkt. Maulid amesema kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ADEM imeweka mikakati ya kuongeza programu za mafunzo, kuimarisha matumizi ya TEHAMA, kupanua tafiti na kuboresha miundombinu katika kampasi zake za Bagamoyo, Mbeya na Mwanza.
ADEM ilianza mwaka 1978 ikiwa na jina la MANTEP (Management Training for Educational Personnel) kabla ya kubadilishwa rasmi mwaka 2001 na kuwa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), ikiwa na jukumu la kuandaa viongozi wenye uwezo wa kusimamia taasisi za elimu kwa ufanisi na uwajibikaji.
Taasisi hiyo inalenga kuwa kituo kinachoongoza katika maendeleo ya uongozi wa elimu barani Afrika na kuchangia kujenga mfumo wa elimu utakaowezesha Tanzania kupata wataalamu wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.



Comments
Post a Comment